Nov 12, 2016 07:55 UTC
  • Ripoti: Nimonia inaua watoto wengi bara Afrika

Asilimia 60 ya vifo milioni 5.9 vya watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka 5 vilivyotokea mwaka jana katika nchi za Afrika na Asia vilitokana na ugonjwa wa kichomi au nimonia.

Utafiti uliofadhiliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na ripoti yake kuchapishwa jana katika jarida la kimataifa la masuala ya afya la Lancet Medical Journal umebainisha kuwa, ugonjwa huo ndio unaosababisha vifo vingi kwa watoto wadogo katika nchi za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Angola, Ethiopia na Nigeria.

Mtoto wa Kiafrika akipewa chanjo

Aidha ripoti hiyo imesema kuwa, licha ya kuwepo chanjo ya ugonjwa huo, lakini katika kila watoto 1000 walio na chini ya miaka mitano, 90 huaga dunia kutokana na nimonia katika nchi za Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Mali, Nigeria, Sierra Leone na Somalia.

Utafiti huo umewataka wazazi katika nchi hizo zilizoathiriwa kuwa makini katika suala la chanjo ya ugonjwa huo pamoja na maradhi ya malaria na kuendesha, mbali na kuzingatia usafi wa maji na vyoo.

Ripoti hiyo imeonya kuwa, huenda dunia isifikie Malengo ya Maendeleo-Endelevu ya Milenia ya Umoja wa Mataifa yanayotaka vifo vya watoto wadogo visizidi 25 kwa kila watoto 1000 kwa kila nchi.

Tags