Kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Ethiopia
Zaidi ya watu elfu 11 wametiwa nguvuni na kuwekwa korokoroni nchini Ethiopia kwa kukiuka sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa nchini humo.
Na hii ni katika hali ambayo mivutano ya kisiasa, malalamiko na upinzani wa wananchi ungali unaendelea kushuhudiwa nchini Ethiopia.
Taddesse Hordofa, mkuu wa tume ya kuchunguza hali ya hatari iliyotangazwa nchini humo ameeleza kupitia taarifa iliyotangazwa na televisheni ya taifa kwamba watu wapatao 11,607 wametiwa mbaroni na kuwekwa korokoroni hadi sasa kuhusiana na kukiuka sheria hiyo ya hali ya hatari, miongoni mwao wakiwemo wanawake 347.
Hordofa ametoa orodha ndefu ya makosa waliyohusishwa nayo watu hao yakiwemo makosa makubwa ya jinai kuanzia 'kushambulia vikosi vya usalama kwa kutumia silaha moto' na 'kuua raia na askari wa usalama' mpaka kosa la 'kuvuruga harakati za misafara ya magari'.
Takwimu hizo zimetolewa katika hali ambayo Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn mwishoni mwa mwezi uliopita wa Oktoba alitangaza idadi ya waliokamatwa kuwa ni watu 2,500.
Mivutano ya kisiasa imeshtadi nchini Ethiopia kwa miezi kadhaa sasa. Japokuwa kwa muda mrefu nchi hiyo imekuwa ikishuhudia manung'uniko ya wananchi yanayotokana na matatizo ya kiuchumi na kijamii, lakini hatua zilizochukuliwa na serikali katika miezi kadhaa ya karibuni ikiwemo ya kuchukua baadhi ya ardhi za kilimo kwa kisingizio cha kupanua mji mkuu Addis Ababa, imekuwa sawa na petroli iliyomiminwa kwenye moto wa malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali hiyo.
Kushadidi malalamiko ya wananchi katika miezi ya karibuni hasa katika maeneo mawili ya Oromo na Amhara na vilvile wito wa vyama vya upinzani wa kuwataka wananchi wapiganie matakwa yao kuliambatana na kuanza hatua za utumiaji nguvu za vyombo vya dola dhidi ya mikusanyiko ya watu kiasi kwamba watu zaidi ya kumi waliuawa na kujeruhiwa katika mikusanyiko ya mwisho ya wananchi iliyofanyika nchini humo.
Tangu tarehe 8 Oktoba serikali ya Addis Ababa imetangaza hali ya hatari katika maeneo hayo mawili ili kudhibiti hali ya mambo na kurejesha usalama, ambapo Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo imetangaza kuwa inafuatilia kwa karibu harakati zozote za mawasiliano na ubadilishanaji tarifa kuhusiana na kufanya maandamano ya kisiasa.
Sambamba na hayo wananchi wamezuiwa na kukatiwa utumiaji wa mitandao yote ya mawasiliano na ya kijamii.
Hata hivyo hatua kali za usalama zilizochukuliwa na vyombo vya dola hazijaweza kuzima moto wa wapinzani. Wananchi na wafuasi wa vyama vya siasa wangali wanaendelea kupigania matakwa yao kwa serikali; na ukatili na utumiaji nguvu kupindukia wa vyombo vya dola umezidisha hasira za wananchi hao.
Japokuwa kutokana na malalamiko makubwa ya wananchi, wiki kadhaa nyuma Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn alichukua hatua ya kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri na hata akachagua mawaziri wawili kutoka kabila la Oromo ili kupunguza joto la upinzani wa watu wa kabila hilo lakini hatua hiyo pia haikuweza kufanikisha lengo hilo.
Wapinzani wanalalamikia pia utendaji wa serikali katika sekta za uchumi na kijamii. Licha ya utajiri mkubwa ilionao Ethiopia, hali ya uchumi wa nchi hiyo haijaboreka hasa baada ya wimbi la ukame kuyaathiri maeneo mengi ya nchi hiyo na kuyafanya yakabiliwe na baa la njaa.
Wapinzani nchini Ethiopia wanasema pia kuwa hakuna uhuru wa kisiasa nchini humo. Kutiwa mbaroni wanaharakati wengi wa kijamii, watumiaji wa mitandao ya intaneti na wanafunzi wa vyuo vikuu kumeifanya hali inayotawala ya mvutano wa kisiasa iwe mbaya zaidi.
Bila ya shaka kupasishwa sheria ya hali ya hatari kwa muda wa miezi sita nchini Ethiopia na kuongezeka uchukuaji hatua za kijeshi katika maeneo ya mijini sio tu si njia mwafaka ya kuzima malalamiko ya wananchi lakini kushtadi wimbi la utiaji nguvuni watu na machafuko kutaifanya hali ya raia wa nchi hiyo iwe ngumu zaidi.
Kutokana na yote hayo tunaweza kusema kuwa kuzingatia matakwa ya wananchi na kujaribu kuyafanyia kazi, kufungua milango ya uhuru wa kisiasa na kufanya mazungumzo na wapinzani kunaweza kupunguza mivutano na hali ya wasiwasi iliyopo na kufungua njia ya kujenga demokrasia na kurejesha amani na usalama nchini humo.../