Jeshi la Algeria: Hatutoshiriki katika jaribio lolote la mapinduzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19846-jeshi_la_algeria_hatutoshiriki_katika_jaribio_lolote_la_mapinduzi
Jeshi la Algeria limetupilia mbali takwa la baadhi ya asasi zinazolitaka kuingilia kati na kumuondoa madarakani Rais Abdelaziz Bouteflika wa nchi hiyo kutokana na maradhi yanayomkabili kwa muda mrefu sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 20, 2016 12:22 UTC
  • Jeshi la Algeria: Hatutoshiriki katika jaribio lolote la mapinduzi

Jeshi la Algeria limetupilia mbali takwa la baadhi ya asasi zinazolitaka kuingilia kati na kumuondoa madarakani Rais Abdelaziz Bouteflika wa nchi hiyo kutokana na maradhi yanayomkabili kwa muda mrefu sasa.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo imelaani mwito huo kuingilia kati mgogoro wa kisiasa na kumuondoa madarakani rais huyo mwenye umri wa miaka 79 kutokana na maradhi na kusema kuwa, kitendo hicho ni njama zilizoshindwa lengo kuu likiwa ni kuleta mpasuko ndani ya jeshi la Algeria. Taarifa ya jeshi hilo imefafanua kuwa, kumuondoa madarakani rais huyo ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

Askari wa Algeria

Rais Abdelaziz Bouteflika alipatwa na ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013 na kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu yaliyochukua muda mrefu. Pamoja na hayo rais huyo aligombea urais katika uchaguzi uliopita licha ya hali yake ya kiafya kuwa mbaya na ambapo aliibuka mshindi. Wakati huo huo, jeshi la nchi hiyo limezionya baadhi ya duru za kisiasa kutumia vibaya hali ya hivi sasa ya nchi hiyo.

Askari wa Algeria katika moja ya maneva ya kijeshi

Ni siku chache zimepita tangu Rais Abdelaziz Bouteflika aliyeingia madarakani mwaka 1999 kurejea nchini humo kutoka Ufaransa alikokwenda kwa ajili ya matibabu.