Wanamgambo wafanya mashambulizi mapya mashariki mwa Kongo DR
Wanamgambo wenye silaha wamefanya mashambulizi katika mkoa wa Tanganyika wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuua na kujeruhi watu kadhaa.
Duru za kijeshi zimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watu watatu wameuawa na wengine wanne kujeruhiwa baada ya wanamgambo wa Pygmée kushambulia eneo la Muswaki katika mkoa wa Tanganyika, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Vile vile wanamgambo wa Pygmée wamechoma moto nyumba za raia katika shambulio lao hilo.
Duru hizo za kijeshi zimesisitiza kuwa, shambulio hilo la wanamgambo wa Pygmée limewafanya wakazi wa eneo la Muswaki kukimbia nyumba zao na kuelekea kwenye aneo la Kalemie la mkoa wa Tanganyika.
Maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanashuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Kushindwa jeshi la nchi hiyo pamoja na askari wa kofia buluu wa Umja wa Mataifa kuwamaliza wanamgambo wenye silaha kumepelekea kuongezeka machafuko na ukosefu wa utulivu katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.