Raia, askari 6 wauawa nchini Mali katika ghasia za uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19951-raia_askari_6_wauawa_nchini_mali_katika_ghasia_za_uchaguzi
Askari watano wa jeshi la Mali na raia mmoja wameuawa na genge la watu waliobeba silaha, wakati walipokuwa wakisafirisha masanduku ya kupigia kura katika mji wa Dilli.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 22, 2016 07:54 UTC
  • Raia, askari 6 wauawa nchini Mali katika ghasia za uchaguzi

Askari watano wa jeshi la Mali na raia mmoja wameuawa na genge la watu waliobeba silaha, wakati walipokuwa wakisafirisha masanduku ya kupigia kura katika mji wa Dilli.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, genge hilo la wabeba silaha, lilitekeleza ukatili huo jana Jumatatu katika mji wa Dilli, kusini magharibi mwa nchi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Mauritania, kwa lengo la kuvuruga uchaguzi wa mabaraza ya miji ya nchi hiyo.

Hata hivyo polisi ya Mali imesema wanamgambo hao hawakufanikiwa kuiba masanduku ya kupigia kura baada ya kuvamia ofisi za manispaa ya mji wa Dilli na kwamba uchaguzi huo kwa ujumla umefanyika chini ya anga tulivu katika maeneo mengi ya nchi.

Uchaguzi wa madiwani Mali

Habari zaidi zinasema kuwa, licha ya uwepo wa vikosi vya kimataifa vya kulinda amani, lakini idadi ndogo ya wapiga kura imeshiriki katika uchaguzi huo wa kuwachagua madiwani 12,000 wa mabaraza ya miji, wakihofia usalama wao.

Haya yanajiri siku chache baada ya askari jeshi mmoja wa kulinda amani wa kikosi cha Umoja wa Mataifa na raia wawili kuuawa katika shambulio linaloshukiwa kufanywa na wanamgambo wenye silaha katika eneo la Mopti, katikati mwa Mali.

Licha ya uwepo wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kilichoko Mali (MINUSMA) ambacho kina wanajeshi na polisi zaidi ya 11,000 kutoka mataifa mbalimbali, lakini magenge ya watu wenye kubeba silaha na makundi ya waasi yamekuwa yakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kilichoko Mali (MINUSMA)