UN: Hali ya kibinadamu nchini Libya inatisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20512-un_hali_ya_kibinadamu_nchini_libya_inatisha
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema, hali ya kibinadamu na kiusalama nchini humo ni ya kutia wasiwasi mkubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 01, 2016 00:39 UTC
  • UN: Hali ya kibinadamu nchini Libya inatisha

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema, hali ya kibinadamu na kiusalama nchini humo ni ya kutia wasiwasi mkubwa.

Martin Kobler amesema, mgogoro wa kiusalama na kibinidamu nchini Libya unatia wasiwasi na kwamba katika kipindi chake chote cha kuhudumu kama mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa hataweza kutatua mgogoro huo bali jukumu la kutatua jambo hilo litakuwa ni la vizazi vijavyo.

Aidha ameelezea kusikitishwa kwake na hatua zilizochukuliwa za kudhibiti wahajiri haramu na kusisitiza kuwa, magendo ya binadamu hayawezi kumalizika nchini humo hadi serikali ya Libya itakapokuwa na nguvu za kweli za kudhibiti kila kitu nchini humo.

Watoto wa Libya, wahanga wakuu wa machafuko ya nchi hiyo

 

Matamshi ya Martin Kobler yametolewa katika hali ambayo kamati ya ngazi za juu ya Umoja wa Afrika iliyoundwa kwa kazi maalumu ya kushughulikia kadhia ya Libya ilisema mwezi uliopita kuwa, mchakato wa kisaisa nchini Libya umekwama kikamilifu na kwamba wanaodhuriwa zaidi na hali hiyo ni wananchi wa kawaida.

Libya imeshindwa kuwa na utulivu tangu alipopinduliwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011 hadi hivi sasa. Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inakabiliwa na migogoro mingi na imegeuka kuwa eneo la kujifichia magenge ya kigaidi, likiwemo kundi la wakufurishaji la Daesh (ISIS).