Rais mteule wa Gambia kuangalia upya suala la kujiondoa ICC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20740-rais_mteule_wa_gambia_kuangalia_upya_suala_la_kujiondoa_icc
Adama Barrow, Rais mteule wa Gambia amesema atatengue uamuzi wa mtangulizi wake aliyembwaga katika uchaguzi wa siku chache zilizopita Yahya Jammeh wa kuiondoa nchi hiyo katika Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 04, 2016 11:36 UTC
  • Rais mteule wa Gambia kuangalia upya suala la kujiondoa ICC

Adama Barrow, Rais mteule wa Gambia amesema atatengue uamuzi wa mtangulizi wake aliyembwaga katika uchaguzi wa siku chache zilizopita Yahya Jammeh wa kuiondoa nchi hiyo katika Mkataba wa Roma uliobuni Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Barrow ambaye alishinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 45 huku Jammeh ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 22 akiambulia asilimia 37 ya kura, amesema kuwa, lengo la ICC ni kuhimiza utawala bora duniani jambo ambalo binafsi analiitakidi.

Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow

Mwezi uliopita, Farhan Haq, Msemaji wa UN alisema Gambia itaacha kuwa mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo ya mjini The Hague kuanzia Novemba 10 mwaka ujao 2017, baada ya nchi hiyo kujiunga na orodha ya nchi kadhaa za Afrika zilizotangaza azma yao ya kujiondoa mahakama hiyo iliyoanza kazi zake Julai mwaka 2002.

Sheriff Bojang, Waziri wa Habari wa Gambia alisema nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika inajiondoa ICC kutokana na kile alichokitaja kuwa, mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi kutumika kama chombo cha kuhujumu na kuwadhalilisha viongozi wa Afrika.

Mbali na kadhia hiyo ya ICC, Rais mteule wa Gambia amesema atawaachia huru wafungwa wote wa kisiasa akisitiza kuwa wakati wa siasa umekwisha na sasa ni wasaa wake wa kuwahudumia wananchi kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe.

Rais wa Gambia anayeondoka, Yahya Jammeh, akitangaza kukubali kushindwa katika uchaguzi wa Disemba 1

Kadhalika Adama Barrow amewataka wananchi wote wa Gambia walioikimbia nchi kutokana na hali ngumu ya maisha na mbinyo wa utawala wa Jammeh warejee nchini wajenge taifa lao.