Watu 20 wapoteza maisha kwenye mgodi Kongo DR
Wachimba migodi 20 wamefariki dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuwaporomokea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akiongea na waandishi wa habari jana Jumapili, Apollinaire Bulindi, Waziri wa Migodi wa mkoa wa Kivu Kusini amesema mkasa huo ulitokea kutokana na idadi kubwa ya watu kukusanyika katika mgodi huo wakisaka dhahabu.
Amesema ofisi yake haina mamlaka ya kudhibiti uchimbaji migodi katika eneo hilo na kwamba aghalabu ya wanaojihusisha na kazi hiyo hawana vibali na hawajaidhinishwa na vyombo vya dola.
Ajali hiyo ya usiku wa kuamkia jana ilitokea katika Mgodi wa Makungu, wilaya ya Fizi,eneo la Sud Kivu, karibu na mpaka na mkoa wa Tanganyika.
Takwimu zinaonyesha, aghalabu ya madini ya dhahabu yanayochimbwa Kongo DR husafirishwa kimagendo katika nchi za Uganda, Rwanda, Burundi na kisha Dubai huko Imarati.
Hii sio mara ya kwanza kwa wachimba migodi haramu nchini DRC kupoteza maisha yao. Disemba mwaka 2014, watu wasiopungua 15 walipoteza maisha wakiwa ndani ya mgodi haramu huko kusini mashariki mwa nchi.
Aidha Mwezi Agosti mwaka 2012 zaidi ya watu 60 walifariki dunia kwenye mgodi katika eneo la Pangoy, Kaskazini Mashariki mwa Kongo DR.