Taharuki yatanda DRC, milio ya risasi yasikika Kinshasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21769-taharuki_yatanda_drc_milio_ya_risasi_yasikika_kinshasa
Hali ya taharuki imetanda katika maeneo mbali mbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku milio ya risasi ikirindima katika mji mkuu Kinshasa mapema leo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 20, 2016 04:15 UTC
  • Taharuki yatanda DRC, milio ya risasi yasikika Kinshasa

Hali ya taharuki imetanda katika maeneo mbali mbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku milio ya risasi ikirindima katika mji mkuu Kinshasa mapema leo.

Maandamano ya hapa na pale pia yameshuhudiwa tokeo jana nchini humo, kumshinikiza Rais Joseph Kabila ambaye muhula wake wa kuhudumu kisheria unamalizika rasmi leo, aachie madaraka. Aidha maafisa usalama wamewekwa tayari katika kila kona ya mji wa Kinshasa na miji mingine ili kudhibiti hali ya mambo.

Waandamanaji wamesikika wakipiga filimbi na ngoma huku wakiwa wamenyayua kadi nyekundu ishara kuwa muda wa Kabila umemalizika na anafaa kuondoka madarakani mara moja na uchaguzi uitishwe.

Polisi wakiwatia mbaroni waandamanaji Kinshasa

Hii ni licha ya mkuu wa upinzani nchini humo Mzee Etienne Tshisekedi kuliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wapinzani hawatafanya maandamano Jumatatu na Jumanne kama ilivyotazamiwa, ili kuepusha maafa na umwagikaji wa damu nchini humo. Chama tawala na baadhi ya vyama vya upinzani viliafikiana kuwa, Rais Kabila asalie madarakani hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika mwaka 2018, jambo abalo limepingwa vikali na muungano mkuu wa upinzani unaoongozwa na Tshisekedi.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema watu karibu 30 wamekamatwa na polisi mjini Kinshasa na 46 katika miji ya Goma na Bukavu, mashariki mwa nchi, kwa kushiriki maandamano.

Hii ni katika hali ambayo, watu saba wameuawa katika makabiliano baina ya polisi na genge la waasi mashariki mwa Kongo DR.

Rais Joseph Kabila wa DRC

Habari zinasema kuwa, makabiliano hayo ya jana Jumatatu yalianza baada ya genge la waasi kuvamia gereza katika mji wa Butembo, mashariki mwa mkoa wa Kivu Kaskazini, ambapo watano miongoni mwao waliuawa pamoja na afisa wa polisi na askari mmoja wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, raia wa Afrika Kusini.