Hofu ya UN kuhusu machafuko na ghasia DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21823-hofu_ya_un_kuhusu_machafuko_na_ghasia_drc
Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kuhusu machafuko yanayoendelea chini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo zaidi ya watu 113 wakiwemo wapinzani wa kisiasa wa serikali wameripotiwa kukamatwa naaskari wa serikali.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 21, 2016 00:22 UTC
  • Hofu ya UN kuhusu machafuko na ghasia DRC

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kuhusu machafuko yanayoendelea chini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo zaidi ya watu 113 wakiwemo wapinzani wa kisiasa wa serikali wameripotiwa kukamatwa naaskari wa serikali.

Maman Sidikou ambaye ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko DRC ameelezea wasiwasi huo kufuatia kamata kamata inayoendelea kwa siku tatu sasa, huku watu wengine wakiwekwa ndani bila kufunguliwa mashtaka.

Amesema tangu tarehe 16 mwezi huu watu 113 wametiwa korokoroni wakiwemo viongozi wa mashirika ya kiraia, wanahabari na watetezi wa haki za binadamu.

Idadi kubwa ya watu wamekamatwa huko Goma, Kinshasa na Bukavu huku Umoja wa Mataifa ukinyimwa kibali cha kuwezesha kufuatilia hali za watu hao ambao amesema wanakamatwa kwa sababu ya kutoa maoni yao ya kisiasa.

Rais Joseph Kabila

Bwana Sidikou ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa DRC, MONUSCO amesihi mamlaka kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu za watu hao na iweke mazingira mwafaka ya kustahamiliana kisiasa.

Maandamano na machafuko yanaendea nchini humo, kumshinikiza Rais Joseph Kabila ambaye muhula wake wa kuhudumu kisheria unamalizika rasmi jana Jumanne, aachie madaraka. 

Aidha maafisa usalama wamewekwa tayari katika kila kona ya mji wa Kinshasa na miji mingine ili kudhibiti hali ya mambo.

Chama tawala na baadhi ya vyama vya upinzani viliafikiana kuwa, Rais Kabila asalie madarakani hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika mwaka 2018, jambo ambalo limepingwa vikali na muungano mkuu wa upinzani unaoongozwa na Tshisekedi.