Jeshi la Marekani lahitimisha rasmi operesheni zake Sirte, Libya
Jeshi la Marekani limetamatisha rasmi operesheni zake katika mji wa pwani wa Sirte nchini Libya, ambao hivi karibuni ulikombolewa kikamilifu toka mikononi mwa magaidi wa Daesh.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imesema kuwa, Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani imekamilisha operesheni ya jeshi la Marekani mjini Sirte iliyopewa jina la Odyssey Lightning, kuanzia Disemba 19.
Pentagon ilianzisha operesheni hiyo Agosti Mosi, kwa kisingizio cha kuvisaidia vikosi vya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kuwatokomeza wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani imesema kuwa, kikosi chake kimetekeleza mashambulizi 495 dhidi ya ngome za Daesh tokea kianzishe operesheni zake mwezi Agosti.
Mafanikio waliyopata wanajeshi watiifu kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ni pigo kubwa kwa genge la kigaidi la Daesh, ambalo limeudhibiti mji huo wa kistratajia kwa zaidi ya mwaka mmoja. Karibu wanajeshi 700 wa serikali ya Umoja wa Kitaifa wameripotiwa kuuawa katika opereseheni ya kuikomboa Sirte.
Mji wa Sirte ambao upo yapata kilomita 450 mashariki mwa mji mkuu Tripoli, ni sehemu alikozaliwa dikteta aliyeuawa wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.