Umoja wa Mataifa wamtaka Jammeh akabidhi madaraka Gambia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemtaka Rais wa Gambia amkabidhi madaraka kwa amani Rais mteule wa nchi hiyo.
Farhan Haq, msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema leo kuwa Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa umoja huo anayemaliza muda wake, amemtaka Rais Yahya Jammeh amkabidhi madaraka kwa amani Adama Barrow mgombea wa muungano wa upinzani aliyeshinda katika uchaguzi wa rais hivi karibuni huko Gambia.
Ban Ki-moon amewaslisha ombi hilo kwa Jammeh katika mazungumzo aliyofanya na Mahmod Tangara, Mwakilishi wa Kudumu wa Gambia katika Umoja wa Mataifa kujadili hali isiyoridhisha ya kisiasa nchini humo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba lililaani hatua ya Rais wa Gambia ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais na kumtaka aheshimu chaguo la wananchi. Tarehe Tisa mwezi huu Yahya Jammeh alijitokeza na kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, wiki moja baada ya yeye binafsi kukubali kubwagwa katika kinyang'anyiro hicho na Adama Barrow mgombea kutoka muungano wa upinzani. Jammeh ametaka kufanyika uchaguzi mwingine wa Rais huko Gambia.