Viongozi wa kidini Kenya wamtaka Uhuru asiidhinishe marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi
Viongozi wa kidini nchini Kenya wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo asisaini muswada wa marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ambao uliidhinishwa na Bunge la Kitaifa hapo jana.
Baraza la Taifa la Makanisa nchini Kenya NCCK na Baraza Kuu la Waislamu nchini humo SUPKEM yamemtaka Rais Kenyatta kutoidhinisha muswada huo, ili kuepuka kulitumbukiza taifa hilo katika machafuko mengine ya baada ya uchaguzi mwakani, kama ilivyoshuhudiwa mwaka 2007/2008.
Hassan ole Naado, Naibu Katibu Mkuu wa SUPKEM amesema rais anafaa kujiepusha na maslahi ya kisiasa na kuegemea upande mmoja ikija katika suala zito kama la uchaguzi linalohusu pande zote za kisiasa na kusisitiza kuwa, mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi yaliidhinishwa na mrengo mmoja wa kisiasa (yaani kambi ya serikali Bungeni).
Kadhalika viongozi hao wa kidini wamemtaka kinara wa upinzani Raila Odinga kutoa kipaumbele kwa mazungumzo badala ya kuitisha maandamano ya nchi nzima ya kupinga sheria hiyo.
Baada ya Wabunge wa mrengo unaotawala wa Jubilee kupasisha muswada unaotaka kufanyiwa mabadiliko sheria za uchaguzi katika Bunge la Kitaifa hapo jana sambamba na wabunge wa upinzani kutoka nje ya ukumbi wa bunge wakati wa kuupigia kura muswada huo, Odinga alifanya kikao na waandishi wa habari na kusema kuwa, wapinzani watandaa maandamano ya nchi nzima kuanzia Januari 4 mwakani, ili kumshinikiza Rais Kenyatta kutousaini muswada huo na kuwa sheria.
Muswada huo unapendekeza kutumiwa njia ya kawaida ya kupiga kura kwa kutuma sajili ya wapiga kura, iwapo mbinu ya kielekitroniki iliyokua imeafikiwa na kamati maalumu iliyowashirikisha wabunge kutoka mrengo wa serikali na upinzani itafeli, kutokana na changamoto za kieleketroniki na kutofika mawimbi ya intaneti katika kila kona ya nchi.