Umoja wa Mataifa wakataa wito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22021-umoja_wa_mataifa_wakataa_wito_wa_kuwekewa_vikwazo_vya_silaha_sudan_kusini
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepinga wito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini, ambayo inashuhudia mapigano kwa mwaka wa nne sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2016 23:39 UTC
  • Umoja wa Mataifa wakataa wito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepinga wito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini, ambayo inashuhudia mapigano kwa mwaka wa nne sasa.

Katika kikao cha upigaji kura hapo jana, rasimu ya azimio hilo iliyoandaliwa na Marekani ilipata uungaji mkono wa kura 7 pekee kati ya 15, huku nchi 8 zikiwemo Russia, China na Japan zikijizuia kupiga kura.

Ili rasimu ipasishwe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lazima ipigiwe kura tisa na wakati huo huo kusiwe na kura ya veto kutoka moja ya nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza hilo.

Sehemu ya mauaji Sudan Kusini

Nchi zingine zilizojizuia kupiga kura ni Malaysia, Venezuela, Angola, Misri na Senegal, licha ya Marekani, Uingereza na Ufaransa kusisitizia umuhimu wa kukatwa mzunguko wa silaha katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Haya yanajiri siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka kutahadharisha kuwa Sudan Kusini iko katika ncha ya kushuhudia mauaji ya kimbari iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, huku akikariri wito wake wa kutaka nchi hiyo iwekewe vikwazo vya silaha.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu, Ban Ki-moon ambaye siku chache zijazo muda wake wa kuhudumu utamalizika alisema: "Iwapo tutafeli kufanya maamuzi magumu, Sudan Kusini itatumbukia katika mauaji ya kikabila na ya umati. Baraza la Usalama lazima lichukue hatua kuhakikisha kuwa mizizi ya mzunguko wa silaha nchini humo inakatwa."

Rais Salva Kiir (Kushoto) na makamu wake wa zamani, Riek Machar

Yasmin Sooka, Mjumbe wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini hivi karibuni baada ya kurejea kutoka safari ya siku 10 ya kuitembelea nchi hiyo alisema kuwa,  kumetokea mauaji ya kimbari katika maeneo kadhaa ya Sudan Kusini na kwamba kuna uwezekano hali ya nchi hiyo ikawa sawa na ile ya Rwanda mwaka 1994. Hata hivyo, Akuei Bona Malwal, Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa ameyakanusha madai hayo na kusisitiza kuwa, hali sio mbaya kiasi hicho, kama inavyotaka kuonyesha UN.