Raia 13 wauawa DRC mkoani Kivu katika hujuma ya kikabila
Raia 13 wa kabila la Hutu wameuawa leo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kile kilichotajwa kuwa ni hujuma ya kulipiza kisasi iliyofanywa na wanagambo wa kabila la Nande.
Taarifa zinasema, raia hao wa Kihutu wameshambuliwa kwa bunduki na mapanga katika kile kilichotajwa ni ulipizaji kisasi baada ya raia kadhaa wa kabila la Nande kuuawa wiki iliyopita katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Taarifa zinasema kundi la wanamgambo wa kabila la Nande wanaojulikana kama Mai Mai Mazembe mapema leo Jumapili wameshambulia mji wa Nyanzale na kutekeleza ukatili huo. Wanagambo wawili wa kundi hilo pia waliuawa katika mapigano hayo.
Uhasama baina ya makabila unaripotiwa kuongezeka katika eneo hilo kutokana na kuhamahama watu na pia oparesheni za jeshi la DRC dhidi ya wanamgambo wa Kihutu katika eneo hilo.

Uhasama baina ya makundi ya wanamgambo umeongezek katika kipindi cha wiki moja iliyopita huku kukiwa na wasiwasi kuwa hatua ya kuongezwa muda urais wa Joseph Kabila huenda ikazidisha malumbano ya kikabila.
Wiki jana watu 40 walipoteza maisha katika mji mkuu, Kinshasa wakati wa maandamano ya kumtaka Rais Kabila aondoke madarakani. Hivi sasa kunafanyika mazungumzo ya kumruhusu Kabila kuendelea kubakia madarakani hadi mwishoni mwa mwaka 2017.