Makumi ya raia wauawa na wanamgambo wa ADF-Nalu Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22189-makumi_ya_raia_wauawa_na_wanamgambo_wa_adf_nalu_kongo_dr
Makumi ya raia wanaripotiwa kuuawa kufuatia mashambulio ya wanamgambo wa ADF-Nalu wa Uganda katika mkoa wa Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 26, 2016 13:07 UTC
  • Makumi ya raia wauawa na wanamgambo wa ADF-Nalu Kongo DR

Makumi ya raia wanaripotiwa kuuawa kufuatia mashambulio ya wanamgambo wa ADF-Nalu wa Uganda katika mkoa wa Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ripoti zinasema kuwa, raia wasiopungua 32 wameuawa baada ya wanamgambo hao wa ADF-Nalu kufanya mashambulio dhidi ya vijiji kadhaa katika mkoa wa Kivu Kaskazini. 

Amisi Kalonda mmoja wa maafisa wa jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza kuwa, mashambulio ya wanamgambo hao yaliulenga mji wa Eringeti na viunga vya mji wa Beni ulioko kaskazini mwa mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Usalama umeimarishwa DRC ili kukabiliana na wapinzani wa Rais Kabila

Afisa huyo wa kijeshi ameziambia duru za habari kwamba, jeshi la serikali limefanikiwa kuwaua wanamgambo wanne katika mapigano yaliyozuka baina ya pande mbili.

Kwa zaidi ya miaka miwili sasa mkoa wa Kivu Kaskazini umekuwa ukishuhudia mashambulio ya mara kwa mara ya makundi ya wanamgambo. Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, raia wapatao 700 wameuawa hadi sasa kufuatia mlolongo wa mashambulio hayo ya wanamgambo.

Msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mak Hazukay amethibitisha kutokea shambulio hilo la waasi na kubainisha kwamba, licha ya jeshi kufanikiwa kuwaua wachama kadhaa wa kundi la ADF lakini idadi ya raia waliouawa ni kubwa.

Mauaji hayo yaliyofanywa na waasi yanaripotiwa katika hali ambayo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hivi sasa inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa kutokana na uchaguzi wa nchi hiyo kuakhirishwa na muhula wa uongozi wa Rais Kabila kumalizika.