Kenya yatangaza hali ya tahadhari
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2239-kenya_yatangaza_hali_ya_tahadhari
Kenya imetangaza hali ya tahadhari kutokana na wasiwasi wa uwezekano wa kutokea mashambulio ya kigaidi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 01, 2016 12:12 UTC
  • Kenya yatangaza hali ya tahadhari

Kenya imetangaza hali ya tahadhari kutokana na wasiwasi wa uwezekano wa kutokea mashambulio ya kigaidi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Ripoti zilizopo zinaonesha kuwa, baada ya kumalizika mwezi Februari na kuanza mwezi Machi kwa sasa viwanja vya ndege vya nchi hiyo viko katika hali ya tahadhari. Eric Kiraithe, Mkuu wa Usalama wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini Kenya (KAA) amesema kuwa, kutokana na nyaraka walizonazo, kuna uwezekano wanamgambo wa al-Shabab kutekeleza mashambulio ya kigaidi katika viwanja vya ndege vya nchi hiyo. Ametanabahisha kwamba, yamkini mashambulio hayo yakatoa pigo kwa vitengo muhimu na kutishia usalama wa taifa hilo. Kiraithe ameongeza kuwa, kuna kundi la watu 11 ambalo limeandaliwa kwa ajili ya kutekeleza mashambulio ya kujitolea muhanga nchini Kenya na kwamba, watano kati yao wameandaliwa kwa ajili ya kufanya mashambulio hayo dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta au Uwanja wa Ndege wa Wilson. Kenya ambayo ni jirani ya Somalia imekuwa ikiandamwa na mashambulio ya wanamgambo wa al-Shabab kutokana na kupeleka kikosi chake cha wanajeshi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kwa ajili ya kushiriki katika kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika AMISOM ambacho kinaendesha operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo hao. Kenya imetangaza hali ya tahadhari katika hali ambayo, hivi karibuni wanamgambo wa al-Shabab wameshadidisha mashambulio yao huku Somalia. Kundi la al-Shabab ambalo ni tawi la mtandao wa al-Qaeda limekuwa likiendesha operesheni kwa shabaha ya kuiangusha serikali ya Somalia. Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Somalia ikipata himaya ya kimataifa imepigwa jeki baada ya kutumwa nchini humo kikosi cha askari elfu ishirini na mbili cha Umoja wa Afrika. Licha ya wanamgambo wa al-Shabab kupoteza maeneo yake mengi iliyokuwa ikiyadhibiti nchini Somalia, lakini katika miezi ya hivi karibuni wanaonekana kushadidisha mashambulio yao na hivi karibuni walitekeleza shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi ya AMISOM.

Aidha katika miezi ya hivi karibuni wanamgambo wa al-Shabab wamekithirisha mashambulio yao dhidi ya majengo ya serikali na hoteli nchini humo. Licha ya kuendeshwa vita dhidi ya al-Shabab, lakini wanamgambo hao wangali wanadhibiti baadhi ya maeneo nchini Somalia na hivyo kuwa tishio kwa usalama wa nchi hiyo na majirani zake ikiwemo Kenya. Kenya ina wanajeshi zaidi ya elfu nne katika kikosi cha askari elfu 22 wa Umoja wa Afrika huko Somalia na wanajeshi hao wamekuwa wakipigana bega kwa bega na serikali na kuisaidia katika vita dhidi ya wanamgambo hao. Kuweko kikosi cha Kenya huko Somalia na nchi hiyo kuwa na mpaka wa pamoja na Somalia ni jambo ambalo limewafanya wanamgambo wa al-Shabab kupanua wigo wa mashambulio yao.

Mashambulio ya wanamgambo wa al-Shabab nchini Kenya mbali na kusababisha mauaji na vifo dhidi ya raia, yametoa pigo kubwa pia kwa uchumi wa nchi hiyo. Sehemu kubwa ya uchumi wa Kenya inategemea sekta ya utalii na kuongezeka aina yoyote ile ya ukosefu wa usalama katika nchi hiyo ya Afrika mashariki hutoa pigo kubwa kwa muundo wa uchumi na pato la nchi hiyo. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, tishio la hatari ya mashambulio ya kigaidi nchini Kenya katika mwaka huu wa 2016 nalo linahesabiwa kuwa sababu hasi katika ustawi wa uchumi wa nchi.

Inatabiriwa kwamba, vitisho vya ugaidi katika mwaka huu nchini Kenya navyo vitapelekea kupungua ukuaji na ustawi wa uchumi. Hii ni kutokana na kuwa, mbali na kupungua watalii wanaoelekea Kenya, tishio hilo litayafanya mashirika ya kigeni kuwa na kigugumizi katika kushirikiana na serikali ya nchi hiyo.

Tangazo la hali ya hatari na uwezekano wa kufanyika mashambulio ya kigaidi nchini Kenya linatolewa katika hali ambayo, nchi hiyo imekuwa ikipitia tajiriba ya mivutano ya kisiasa na kiusalama na jirani yake Somalia. Aidha mivutano ya kisiasa nchini Kenya nayo imeshika kasi.

Si hayo tu, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limetangaza kuwa, Wakenya milioni tatu wanahitajia misaada ya chakula. Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, kutokana na mazingira haya inaonekana kuwa, nchi jirani zinapaswa kuweka kando hitilafu zao na kutekeleza siasa za pamoja dhidi ya ugaidi katika eneo kwa shabaha ya kuliangamiza kundi la wanamgambo wa al-Shabab.