Morocco yaanza kutekeleza mfumo wa Benki za Kiislamu
Serikali ya Morocco imejiunga na mfumo wa Benki za Kiislamu kwa kuanzisha benki tano za Kiislamu nchini humo.
Shirika la habari la Associated Press limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, uamuzi huo umechukuliwa ili kwenda sambamba na ongezeko na ustawi wa mfumo wa Benki za Kiislamu na vile vile kutekeleza ahadi za chama cha Kiislamu cha Morocco ambacho kinaongoza serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo.
Huko nyuma Morocco ilikuwa haisemi lolote kuhusiana na mfumo wa kibenki wa Kiislamu lakini hivi sasa baada ya kuingia madarakani chama chenye mielekeo ya Kiislamu na kustawi mfumo wa Benki za Kiislamu, nchi hiyo ya Kiarabu imeonesha hamu kubwa ya kutumia mfumo huo.
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, kutoa au kupokea riba ni haramu, wakati msingi mkuu wa benki nyingi duniani ni riba katika uendeshaji wake.
Chama cha Uadilifu na Ustawi cha Morocco kiliahidi mwaka 2011 kwamba kitaanzisha Benki za Kiislamu nchini humo.
Inaonekana kuwa, hivi sasa chama hicho kimeamua kuingia kikamilifu kwenye mfumo wa kibenki wa Kiislamu, kwa kuanzisha benki hizo tano za Kiislamu huko Morocco.