Kundi Jingine la upinzani DRC lajiunga na mkataba wa amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22930-kundi_jingine_la_upinzani_drc_lajiunga_na_mkataba_wa_amani
Huko nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, jukwaa la kuheshimu katiba ya nchi hiyo limetangaza litatia saini makubaliano ya kisiasa yaliyotiwa siani hivi karibuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2017 04:29 UTC
  • Kundi Jingine la upinzani  DRC lajiunga na mkataba wa amani

Huko nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, jukwaa la kuheshimu katiba ya nchi hiyo limetangaza litatia saini makubaliano ya kisiasa yaliyotiwa siani hivi karibuni.

Mratibu wa jukwaa hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha MLC, Eve Bazaïba, aliyasema hayo Alhamisi mjini Kinshasa baada ya mkutano na viongozi wa jumuiko la maaskofu nchini humo,  CENCO ambao wanapatanisha pande hasimu nchini humo.

Bi. Bazaïba amesema wamefikia hatua hiyo baada ya wasuluhishi kutambua madai yao, akieleza kuwa hoja yao ni kushika madaraka kwa mujibu wa katiba na si vinginevyo.

Kitendo cha jukwaa hilo kukubali kujumuika kwenye makubaliano hayo yaliyopitishwa tarehe 31 mwezi uliopita kinaendeleza wito wa Umoja wa Mataifa wa kutaka pande zote kinzani huko DRC kushiriki kwenye mchakato huo kwa maslahi ya wananchi wote.

Maandamano ya wapinzani mjini Kinshasa

Hiyo juzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitaka kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya kukabidhi madaraka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa mapatano hayo ya Disemba 31, Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo amekubali kung'atuka uongozini mwishoni mwa mwaka huu wa 2017.

Zaidi ya watu 40 wamepoteza maisha katika siku za hivi karibuni, katika maandamano ya kutaka Kabila aondoke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo tokea mwaka 2001 wakati baba yake, Laurent Desire Kabila, alipouawa.