Kutangaza vita "Walipizaji Kisasi wa Niger Delta" dhidi ya serikali ya Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23047-kutangaza_vita_walipizaji_kisasi_wa_niger_delta_dhidi_ya_serikali_ya_nigeria
Katika hali ambayo Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameahidi kufikia suluhu na waasi, kundi la wana mgambo linalojiita Walipizaji Kisasi wa Niger Delta la kusini mwa nchi hiyo limetangaza vita dhidi ya serikali baada ya mazungumzo baina ya pande mbili kumalizika bila ya kufikiwa tija.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jan 08, 2017 02:48 UTC
  • Kutangaza vita

Katika hali ambayo Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ameahidi kufikia suluhu na waasi, kundi la wana mgambo linalojiita Walipizaji Kisasi wa Niger Delta la kusini mwa nchi hiyo limetangaza vita dhidi ya serikali baada ya mazungumzo baina ya pande mbili kumalizika bila ya kufikiwa tija.

Taarifa iliyotolewa na kundi la Walipizaji Kisasi wa Niger Delta imewataka wapiganaji wote na makamanda wa kundi hilo wajiweke tayari kikamilifu kwa mapambano. Mnamo mwaka uliopita kundi hilo lilishadidisha mashambulio dhidi ya vinu na mabomba ya mafuta kusini mwa Nigeria. Mashambulio hayo yalisababisha hasara kwa vinu na mabomba mengi ya mafuta na kupunguza kiwango cha usafirishaji nje mafuta ya nchi hiyo. Katika mwaka huo wa 2016 usafirishaji wa mafuta ghafi ya Nigeria ulipungua kutoka mapipa milioni mbili na laki moja kwa siku hadi mapipa takribani milioni moja na laki nane. Uuzaji mafuta ghafi unaipatia Nigeria theluthi mbili ya pato la fedha za kigeni; na kupungua uzalishaji, sambamba na kushuka bei ya bidhaa hiyo umepelekea kuzorota kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi hiyo.

Hujuma dhidi ya vinu na mabomba ya mafuta katika eneo la Niger Delta

Mwaka uliopita 2016, na baada ya kufanya mashambulio na hujuma kadhaa zilizoharibu vinu vya mafuta, kundi la Walipizaji kisasi wa Niger Delta lilitangaza usitishaji vita ili kutoa fursa ya kufanya mazungumzo na serikali juu ya namna ya kulipatia eneo la Niger Delta fungu kubwa zaidi la pato linalotokana na uuzaji mafuta, lakini mazungumzo hayo hayakukidhi matarajio ya kundi hilo. Tangu miezi sita iliyopita serikali ya Nigeria ilianzisha mazungumzo na viongozi wa kundi hilo kwa madhumuni ya kupunguza kiwango cha umasikini na uchafuzi wa mazingira unaotokana na mafuta katika eneo la Niger Delta la kusini mwa nchi hiyo lakini kundi la Walipizaji kisasi  wa Niger Delta linalalama kuwa mazungumzo hayo hayajazaa matunda yoyote. Kundi hilo limetangaza vita katika hali ambayo Rais Muhammadu Buhari alitangaza katika salamu za mwaka mpya wa 2017 azma ya kufikia suluhu na kurejesha amani katika eneo la Niger Delta na akasisitiza kwamba serikali yake imekusudia katika mwaka huu kufikia suluhu ya kudumu na waasi wa eneo hilo.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria

Makundi ya waasi ya eneo la Niger Delta yanataka kugawanywa pato la mafuta kwa wananchi na kuongezwa fungu la eneo hilo la mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa hiyo. Niger Delta ni moja ya maeneo yenye uchafuzi mkubwa zaidi wa mazingira duniani. Kuweko mabomba ya mafuta ya urefu wa kilomita zipatazo elfu saba na hujuma za mara kwa mara zinazofanywa dhidi ya mabomba hayo kumesababisha kumwagika mafuta katika mito iliyoko katika maeneo ya misituni na hivyo kuchafua na kuyafanya yasiweze kutumika maji na viumbe vya mitoni na baharini vya eneo hilo. Kiwango cha juu zaidi cha gesi hatari ya sumu (greenhouse gases) duniani inazalishwa katika eneo la Niger Delta.

Wanamgambo wabeba silaha katika eneo la Niger Delta

Kila mwaka tani milioni thelathini na tano za gesi ya kaboniki zinachafua hali ya hewa ya eneo hilo. Yote hayo ni miongoni mwa mambo yaliyowakatisha tamaa wakaazi wa eneo la Niger Delta na kuchochea harakati za makundi ya waasi katika eneo hilo. Mgogoro wa eneo lenye utajiri wa mafuta la kusini mwa Nigeria umeshtadi katika hali ambayo viongozi wa serikali ya Abuja wanakabiliwa na matatizo ya kupungua pato linalotokana na  mafuta, mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haramu katika maeneo ya kaskazini, magendo ya bidhaa na uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo…/