Siku elfu moja zimepita tangu kutekwa wanafunzi wa Chibok Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23107-siku_elfu_moja_zimepita_tangu_kutekwa_wanafunzi_wa_chibok_nigeria
Ikiwa zimepita siku elfu moja hapo jana Jumapili tangu kutekwa wanafunzi wa kike wa shule ya sekondari ya Chibok zaidi ya 200 kulikofanywa na wanamgambo wa kundi la kitakfiri na la kigaidi la Boko Haram huko Nigeria, hatima ya wanafunzi hao haijulikani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 09, 2017 04:33 UTC
  • Siku elfu moja zimepita tangu kutekwa wanafunzi wa Chibok Nigeria

Ikiwa zimepita siku elfu moja hapo jana Jumapili tangu kutekwa wanafunzi wa kike wa shule ya sekondari ya Chibok zaidi ya 200 kulikofanywa na wanamgambo wa kundi la kitakfiri na la kigaidi la Boko Haram huko Nigeria, hatima ya wanafunzi hao haijulikani.

Ripoti iliyotolewa jana na redio ya kimataifa ya Ufaransa imeeleza kuwa, hii leo zimepita siku elfu moja tangu kutekwa wanafunzi wa kike wa shule ya sekondari ya Chibok wapatao 276. Wanafunzi hao walitekwa na wanamgambo wa kundi la Boko Haram huko Chibok katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria. Mabinti hao walitekwa nyara na Boko Haram Aprili 14 mwaka 2014.

Baadhi ya mabinti hao wamefanikiwa kutoroka na wengine kuokolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram kufuatia oparesheni za jeshi la Nigeria, hata hivyo mabinti wengine 195 hadi sasa wanaendelea kushikiliwa na kundi hilo.

Baadhi ya wanafunzi waliokuwa wametekwa nyara na Boko Haram wakizungumza na Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria

Aisha Yusufu Makamu, Mkuu wa harakati inayofuatilia wanafunzi hao ijulikanayo kwa jina la " Bring Back Our Girls" amesema kuwa, hatima ya mabinti wengi hadi sasa haijulikani na kwamba kukubali ukweli kuwa, hadi sasa zimepita siku elfu moja tangu kutekwa nyara wanafunzi hao si jambo jepesi. Kundi la wakufurishaji la Boko Haram linaendesha hujuma na jinai mbalimbali huko Nigeria tangu mwaka 2009.