Boko Haram washambulia kituo cha jeshi la Nigeria, askari watano wauawa
Askari watano wa jeshi la Nigeria na wapiganaji 15 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wameuawa wakati kundi hilo liliposhambulia kituo cha jeshi katika eneo la mbali kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la Nigeria hapo jana imeeleza kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram siku ya Jumamosi walishambulia brigedi ya jeshi iliyopo eneo la Buni Yadi katika jimbo la Yobe.
Duru moja ya jeshi la Nigeria imeripoti kuwa "wanajeshi watano walipoteza maisha yao katika shambulio japokuwa wanamgambo zaidi ya 15 wa Boko Haram waliuliwa na askari hao".
Wakati huohuo sauti kadhaa za miripuko zilisikika jana katika mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno, eneo ulipoanzia uasi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram miaka saba iliyopita na kusababisha watu wasiopungua 15,000 kuuawa na wengine zaidi ya milioni mbili kubaki bila ya makaazi.
Kundi hilo lilikuwa limedhibiti sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria, lakini tangu mapema mwaka jana limetimuliwa kwenye karibu maeneo yote na jeshi la serikali likisaidiwa na vikosi vya mataifa jirani.
Jeshi la Nigeria lilitangaza mwezi uliopita kuwa limeiteka na kuisambaratisha ngome kuu ya Boko Haram katika msitu wa Sambisa, hata hivyo tangu kutolewa taarifa hiyo kundi hilo limeendelea kufanya mashambulio ya kujitoa mhanga.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema, uwezo wa Boko Haram kufanya mashambulio katika nchi jirani za Niger, Cameroon na Chad unaashiria kuwa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri lina ngome na vituo kadhaa vya kijeshi…/