Raia zaidi ya milioni mbili wa Sudan Kusini wakimbilia nchi jirani
Raia wengi wa Sudan Kusini wamelazimika kuihama nchi hiyo na kukimbilia katika nchi jirani kutokana na mgogoro wa kisiasa na mauaji yanayoendelea nchini humo.
Ofisi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) huko Kinshasa mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kuwa, wahajiri wa Sudan Kusini zaidi ya milioni mbili mwaka jana walikimbilia Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kupata hifadhi.
Eric Ngala mmoja wa maafisa wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema kuwa kiasi hicho kinahesabiwa kuwa kikubwa zaidi cha wahajiri kuwahi kushuhudiwa barani Afrika tangu baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.
Sababu kuu iliyowalazimisha raia hao wa Sudan Kusini kuihama nchi yao ni vita vya ndani vilivyoikumba nchi hiyo kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa Makamu wake, Riek Machar.
Ni zaidi ya miaka mitatu ambapo vita vya ndani vinaendelea nchini Sudan Kusini. Baadhi ya ripoti za kimataifa zinasema kuwa kinafanyika mauaji ya kimbari nchini Sudan Kusini. Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi wa nchi hiyo Riek Machar mwezi Agosti mwaka juzi walisaini makubaliano ya amani kufuatia kuvurugika hali ya mambo nchini humo. Hata hivyo mauaji yangali yanaendelea nchini humo licha ya kufikiwa mwafaka na makubaliano ya amani.
Hali imekuwa mbaya zaidi nchini Sudan Kusini kutokana na ongezeko la raia wa nchi hiyo wanaokimbilia katika maeneo ya mpakani karibu na nchi jirani. Raia wengi wa Sudan Kusini wanaishi makambini kwenye mipaka ya nchi hiyo na nchi jirani kutokana na hali ngumu ya kimaisha.
Hii ni katika hali ambayo hali ya kisiasa na kiuchumi katika nchi jirani na Sudan Kusini si ya kuridhisha. Kwa mfano tu nchi ya Sudan kwa sasa inasumbuliwa na matatizo mengi ya kisiasa ya kiuchumi na mzozo wa mipaka, masuala ambayo yamewafanya wakimbizi wengi waishi katika mazingira magumu. Katika mipaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia hali ni hiyo hiyo.
Katika mazingira hayo, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ameagiza iundwe kamati ya watu 30 katika juhudi za kufanikisha mapatano ya kitaifa na kuishirikisha serikali katika utekelezaji wa makubaliano ya amani kati yake na upande wa upinzani.
Hali ya mambo ya Sudan Kusini imekuwa mbaya sana kiasi kwamba, raia wengi wa nchi hiyo wanafanya mikakati ya kukimbilia nje ya nchi. Vilevile ripoti zinaonesha kwamba, raia wengi wa Sudan Kusini wanasumbuliwa na hatari ya kifo kutokana na na ukame na uhaba wa huduma za afya na tiba.