Wafanyakazi wa sekta ya mafuta na gesi nchini Nigeria wagoma kudai mshahara
Wafanyakazi wa sekta ya mafuta na gesi nchini Nigeria, wameanzisha mgomo kulalamikia kutolipwa mishahara na marupurupu yao.
Mgomo huo uliowahusisha wafanyakazi wa sekta tofauti za gesi na mafuta katika jimbo la Delta, kusini mwa Nigeria, ulianza Jumanne ya jana. Baadhi ya duru za habari zimeripoti kuwepo uwezekano wa mgomo huo kuendelea kwa siku kadhaa, kuishinikiza serikali ya Rais Muhammadu Buhari itekeleze matakwa yao.
Katika hali ambayo sekta ya mafuta na gesi nchini Nigeria kwa kipindi kirefu imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya makundi ya wabeba silaha na magaidi hususan katika eneo la Delta, hivyo mgomo mpya unatazamiwa kuifanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi kwenye sekta hizo.
Katika miaka ya hivi karibuni uzalishaji mafuta nchini Nigeria ambayo ni mzalishaji mkubwa wa nishati hiyo barani Afrika, umeshuka kwa karibu thuluthi moja na hivyo kuufanya uchumi wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika kuwa mbaya zaidi.