Umoja wa Afrika waitishia Gambia
Mgogoro wa kisiasa nchini Gambia umekuwa tata zaidi katika kukaribia tarehe ya kuapichwa rais mpya wa nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo Umoja wa Afrika (AU) umemtishia Rais wa Gambia kuwa hautamtambua rasmi kuwa rais halali tangu tarehe iliyoanishwa kwa ajili ya kufanyika sherehe za kumuapisha rais mteule wa nchi hiyo.
Umoja wa Afrika umetoa matamshi makali kwa Rais Yahya Jammeh wa Gambia huku mashauriano yakiendelea ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo. Kundi linaloundwa na wakuu kadhaa wa nchi za Kiafrika hivi karibuni lilifanya safari huko Banjul mji mkuu wa Gambia katika jitihada za kuindoa nchi hiyo katika hali ya mgogoro. Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ndiye aliyeongoza ujumbe huo wa viongozi wa Afrika mjini Banjul. Katika safari hiyo, Rais Buhari alifuatana na Rais Ellen Johnson Sirleaf wa LIberia na John Dramani Mahama, rais wa zamani wa Ghana. Baada ya mazungumzo yao, ujumbe huo ulisema unataraji kuwa ufumbuzi wa mgogoro wo Gambia utapatikana.
Mgogoro wa kisiasa umepamba moto huko Gambia baada ya kutangazwa mshindi aliyekuwa hasimu wa Rais Jammeh katika uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini humo.Yahya Jammeh ambaye amekuwa madarakani kwa muda wa miaka 22 awali alikubali kushindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe Mosi Disemba mwaka jana, hata hivyo baadaye alibadili msimamo wake na kupinga matokeo hayo; hatua iliyoibua makelele na malalamiko ya jamii ya kimataifa. Hofu imetanda sasa huko Gambia kuhusu uwezekano wa kushtadi mgogoro nchini huku raia wengi wakiikimbia nchi wakihofia kutokea vita nchini humo. Katiba ya Gambia inaeleza kuwa, Jammeh anapasa kukabidhi madaraka kufikia Januari 19; huku sherehe za kuapishwa Rais Mteule Adama Barrow zikiwa zimepangwa kufanyika pia tarehe hiyo hiyo.
Hali inazidi kulegalega huko Gambia huku Rais Jammeh akiendelea kung'ang'ania kubaki madarakani. Mashauriano yaliyofanyika hadi sasa hayajazaa matunda. Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi ya Gambia ametoroka nchi na Mahakama Kuu imetangaza kuwa hakuna majaji wa kuchunguza malalamiko yaliyowasilishwa na Yahya Jammeh kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi. Hii ni katika hali ambayo jeshi la Gambia linasisitiza kufungamana na Jammeh. Hata hivyo nje ya Gambia, nchi za Magharibi mwa Afrika na taasisi za kieneo zinafanya juhudi za kurejesha demokrasia na kuzuia kutokea vita nchini humo. kwa upande wake Rais Mteule wa Gambia amewataka wafuasi wake wasiitumbukize hatarini amani na utulivu wa nchi hiyo. Wakati huo huo inaonekana kuwa iwapo mashauriano ya sasa hayatazaa matunda si Umoja wa Afrika na taasisi za kieneo pekee ndizo zitakazomchukulia hatua Yahya jJammeh, bali makabiliano ya wapinzani na chama tawala yatazusha vita vingine katika eneo. Umoja wa Afrika ambayo ni taasisi kuu ya nchi za Kiafrika inayotekeleza majukumu yake kufanikisha malengo makubwa ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii kwa ajili ya kudumisha amani na uthabiti ndani ya bara hilo na vile vile kuimarisha nafasi ya Afrika kimataifa, imemuonya Jammeh. Zimesalia siku chache tu kabla ya kumalizika muhula wa kuhitimishwa hali hiyo ya mambo huko Gambia. Jammeh anapasa kukubali kung'atuka madarakani au kinyume chake nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikabiliwe na wimbi la mauaji. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa kieneo wanasisitiza kuwa utumiaji nguvu dhidi ya serikali ya Gambia unapasa kuwa chaguo la mwisho na kwamba uainishwe muhula ili njia zote za kidiplomasia zitumike kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.