Waislamu Nigeria wawaonya viongozi wa nchi hiyo
Msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amewaonya viongozi wa nchi hiyo na kuwataka wamwachie huru mara moja kiongozi wa harakati hiyo.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Ibrahim Musa, msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria akisema jana katika tamko la jumuiya hiyo kwamba mahakama ya nchi hiyo imetoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaki, lakini hadi hivi sasa viongozi wa nchi hiyo wamekataa kumwachilia huru na wanafanya njama za kuchafua sura ya harakati hiyo.
Msemaji wa Jumuiya ya Kiislamu ya Nigeria ameongeza kuwa, taarifa zilizofichuliwa na duru za kuaminika zilizo karibu na taasisi za kiusalama za Nigeria zinaonesha kuwa, kuna mkono wa nje unaochochea kutotekelezwa amri ya mahakama ya kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Hivi karibuni maafisa usalama wa Nigeria wamemhamishia Sheikh Zakzaki na mkewe katika sehemu isiyojulikana, zikiwa ni njama za kukwepa kutekeleza amri ya mahakama ya kuwaachilia huru.
Kwa mujibu wa amri hiyo ya mahakama, viongozi wa Nigeria wanawajibika kumkabidhi kwa polisi Sheikh Zakzaki katika kipindi cha siku 20 zijazo na jeshi la polisi nalo lina wajibu wa kumwachia huru yeye na mkewe katika kipindi cha masaa 24 tangu watakapokadhibiwa.