Mar 03, 2016 14:08 UTC
  • Watu 24 waaga dunia katika mafuriko nchini Angola

Kwa akali watu 24 wamepoteza maisha huku makumi ya wengine wakitoweka kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Angola.

Habari zinasema kuwa, aghalabu ya walioaga dunia katika janga hilo la kimaumbile ni watoto wadogo, baada ya mto Capitao kuvunja kingo zake na kuwasweka, karibu na soko la Lubango, kusini mwa nchi hiyo. Shirika la habari la Angop limeripoti kuwa, zaidi ya watu 30 hawajulikani waliko tangu mvua hizo zianze kunyesha mapema wiki hii.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, mwezi Machi mwaka jana 2015, watu 64 walifariki dunia wakiwemo watoto wadogo kufuatia mafuriko makubwa yaliyotokea magharibi mwa Angola.

Nchi ya Angola ilikumbwa pia na mafuriko kama hayo mwaka 2009 na 2013.

Aidha Januari mwaka jana, raia wapatao milioni moja wa nchi za Msumbiji, Malawi, Madagascar na Zimbabwe waliathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za el-Nino.

Tags