Morocco: Jammeh astaafu baada ya kumalizika muda wake wa urais
Serikali ya Morocco imemtaka Rais Yahya Jammeh wa Gambia atumie fursa iliyopo kustaafu kwa amani baada ya kumalizika muhula wake wa uongozi.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Morocco imempa pendekezo hilo Rais Jammeh na kuongeza kuwa, iko tayari kumpa hifadhi baada ya kumalizika muda wake. Kwa mujibu wa taarifa hiyo Rabat sanjari na kumtuma mjini Banjul Nasser Bourita, mwakilishi wa Waziri wa Mashauri katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco na Yassine Mansouri, Mkuu wa Vyombo vya Upelelezi nchini humo, imemtaka Rais Jammeh kukubali pendekezo hilo ililolitaja kuwa ni fursa ya dhahabu.

Mgogoro wa Gambia uliibuka baada ya Rais Yahya Jammeh kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mpinzani wake Adama Barrow, ambayo awali aliyakubali. Wakati huo huo rais mteule wa Gambia amesema kuwa, sherehe za kuapishwa kwake kama rais mpya wa nchi hiyo zinapaswa kufanyika kama ilivyopangwa. Adama Barrow ambaye kwa sasa yuko nchini Senegal, amesema sherehe za kuapishwa kama rais mpya wa Gambia zinapaswa kufanyika Alkhamisi ya kesho tarehe 19 Januari kwa mujibu wa katiba ya Gambia.

Hii ni katika hali ambayo Rais Yahya Jammeh kwa upande wake ametangaza hali ya hatari nchini humo kwa siku 90 akiashiria kuingiliwa na nchi ajinabi uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliofanyika mwezi Disemba mwaka jana.