UN kuchunguza uvunjaji sheria wa maafisa wake Darfur Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24022-un_kuchunguza_uvunjaji_sheria_wa_maafisa_wake_darfur_sudan
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, unafanya uchunguzi kuhusu madai kwamba maafisa wake wa kulinda amani katika eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan, wamehamisha silaha kinyume cha sheria.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 21, 2017 10:18 UTC
  • UN kuchunguza uvunjaji sheria wa maafisa wake Darfur Sudan

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, unafanya uchunguzi kuhusu madai kwamba maafisa wake wa kulinda amani katika eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan, wamehamisha silaha kinyume cha sheria.

Shirika la habari la Ufaransa limemnukuu msemaji wa timu ya maafisa wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika akisema kuwa, askari wa kikosi kimoja cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa walihamisha silaha na vifaa vya kijeshi wakati walipokuwa wanaondoka Darfur.

Msemaji huyo ameongeza kuwa, askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika waliwajulisha haraka jambo hilo maafisa wa Sudan na uchunguzi kuhusu jambo hilo ukaanza mara moja.

Wahanga wakuu wa machafuko na usambazaji silaha kiholela huko Darfur ni watoto na raia wa kawaida

 

Maafisa wa timu za kulinda amani za Umoja wa Mataifa hawana ruhusa ya kuondoka Darfur wakiwa na silaha ambazo hazikuorodheshwa. Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa timu ya maafisa hao wa Umoja wa Mataifa ilikuwa inahamisha silaha kwa siri kutoka Darfur. Haikujulikana silaha hizo zilikuwa zinatokea wapi.

Mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliongeza muda wa kazi za maafisa wake wa kulinda amani huko Darfur hadi mwezi Julai mwaka huu wa 2017.