Burundi yawaachia huru mamia ya wafungwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24151-burundi_yawaachia_huru_mamia_ya_wafungwa
Serikali ya Burundi imewaachia huru mamia ya wafungwa kufuatia agizo la Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo, huku watetezi wa haki za binadamu wakidai kuwa hiyo ni njama ya kutoa nafasi ya kukamatwa wanaharakati wa kisiasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 24, 2017 08:09 UTC
  • Burundi yawaachia huru mamia ya wafungwa

Serikali ya Burundi imewaachia huru mamia ya wafungwa kufuatia agizo la Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo, huku watetezi wa haki za binadamu wakidai kuwa hiyo ni njama ya kutoa nafasi ya kukamatwa wanaharakati wa kisiasa.

Aimee Laurentine Kanyana, Waziri wa Sheria wa Burundi amesema kundi la kwanza la wafungwa 300 waliachiwa huru jana Jumatatu, waliokuwa wanatumikia vifungo tofauti katika gereza la Mpimba jijini Bujumbura.

Ameongeza kuwa, miongoni mwa wafungwa walioachiwa huru jana ni wanaharakati 58 waliokamatwa wakishiriki maandamano yaliyokuwa yamepigwa marufuku na serikali Aprili 2014.

Polisi wakikabiliana na waandamanaji Burundi

Waziri wa Sheria wa Burundi amebainisha kuwa, serikali inapania kuwaachia huru wafungwa 2,500 kati ya 10,000, kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana.

Hata hivyo, Pierre-Claver Mbonimpa, afisa wa kundi la kutetea haki za wafungwa la Aprodeh prisoners' defence, amepongeza hatua hiyo na kusisitiza kuwa, serikali lazima iwaachie huru wafungwa wa kisiasa zaidi ya elfu 4 waliokamatwa tangu mgogoro wa Burundi uanze, Aprili 2015.   

Jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu zimekuwa zikilalamika kuwa, serikali ya Bujumbura inatumia siasa za kueneza woga na hofu baina ya wananchi na kwamba mwenendo wa kuuawa, kutoweka na kukamatwa raia bado unaendelea nchini humo.