Equatorial Guinea yaafiki kumpa hifadhi Yahya Jammeh
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24233-equatorial_guinea_yaafiki_kumpa_hifadhi_yahya_jammeh
Viongozi wa Equatoria Guinea wametangaza kuwa wamekubali kumpa hifadhi Rais wa zamani wa Gambia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 25, 2017 14:55 UTC
  • Equatorial Guinea yaafiki kumpa hifadhi Yahya Jammeh

Viongozi wa Equatoria Guinea wametangaza kuwa wamekubali kumpa hifadhi Rais wa zamani wa Gambia.

Serikali ya Equatoria Guinea imesema leo kuwa Rais Teodoro Obiang Nguema wa nchi hiyo amelitaarifu Baraza la Mawaziri kuwa amekubali kumpokea Yahya Jammeh Rais wa zamani wa Gambia kama shakhsia aliyebaidishwa kisiasa. Serikali ya Equatorial Guinea imesisitiza kuwa Rais Obiang amemtaka Jammeh ajiepushe na hatua yoyote ya uchochezi dhidi ya nchi yake katika kipindi atakachokuwa uhamishoni nchini humo. Serikali ya Equatorial Guinea pia imetoa hakikisho la kumdhaminia Yahya Jammeh mazingira ya amani na utulivu akiwa nchini humo.

Yahya Jammeh akielekea uhamishoni Equatorial Guinea 

Baada ya wiki sita za kujiri mgogoro mkubwa wa kisiasa uliosababishwa hatua ya Yahya Jammeh ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni huko Gambia, hatimaye Jammeh amekubali kumkabidhi madaraka Adama Barrow mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi wa Disemba Mosi mwaka jana nchini humo kufuatia mashinikizo ya kimataifa na kutishiwa kijeshi na nchi za Magharibi mwa Afrika. Rais wa zamani wa Gambia anatuhumiwa kwa ufisadi na kuchukua fedha katika hazina ya serikali wakati akiondoka nchini humo.

Wakati huo huo Amie Bojang  aliyetajwa kuwa mshauri wa ngazi ya juu wa Rais Adama Barrow amesema kuwa rais huyo ambaye Ijumaa iliyopita aliapishwa kuwa rais mpya katika sherehe zilizofanyika katika ubalozi wa Gambia mjini Dakar Senegal, kesho Alhamisi alasiri atarejea Gambia.