Kwa mara nyingine mahakama ya Nigeria yataka kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24557-kwa_mara_nyingine_mahakama_ya_nigeria_yataka_kuachiliwa_huru_sheikh_zakzaky
Mahakama Kuu ya Shirikisho la Nigeria, kwa mara nyingine tena imetoa amri ya kuachiliwa huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo na mke wake.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 01, 2017 12:12 UTC
  • Kwa mara nyingine mahakama ya Nigeria yataka kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky

Mahakama Kuu ya Shirikisho la Nigeria, kwa mara nyingine tena imetoa amri ya kuachiliwa huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo na mke wake.

Shirika la habari la Fars limevinukuu vyombo vya habari vya nchini Nigeria vikitangaza habari hiyo na kuitaka Wizara ya Intelijensia na Usalama wa Taifa DSS ya nchi hiyo kumwachilia huru mara moja Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake na kumpeleka sehemu iliyo salama kwa kuishi.

Mahakama Kuu ya Nigeria imeiandikia barua wizara hiyo na kuonya kwamba, kama Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ibrahim Idriss na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Shirikisho la Nigeria AGF Abubakar Malami watakaidi amri ya mahakama ya kumwachilia huru Sheikh Zakzaky na mkewe, basi watakuwa wamefanya kosa la kisheria na wawe tayari kubeba majukumu ya kupinga amri ya mahakama.

Waislamu wa Nigeria wakiandamana kutangaza uungaji mkono wao kwa Kiongozi wa Harakani ya Kiislmu ya nchi hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky

 

Tarehe 2 Disemba 2016 pia, Mahakama Kuu ya Shirikisho la Nigeria ilitoa amri kwa Wizara ya Usalama wa Taifa ya nchi hiyo ya kumwachilia huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa amri hiyo ya mahakama, Sheikh Zakzaky ilibidi aachiliwe huru tarehe 20 mwezi ulioisha wa Januari, lakini wizara hiyo ya serikali ya Rais Muhammadu Buhari imekataa kutekeleza amri hiyo ya mahakama.

Mwezi Disemba 2015, Sheikh Ibrahim Zakzaky alipigwa risasi na kukamatwa na jeshi la Nigeria baada ya jeshi hilo kuua kundi la Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo. Hadi hivi sasa Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu yuko mikononi mwa maafisa usalama wa Nigeria.