Nigeria yaahidi kuwapatia malipo yaliyocheleweshwa wanamgambo wa zamani wa Niger Delta
Serikali ya Nigeria imesema, karibuni hivi italipa fedha zote za malipo yaliyocheleweshwa inazodaiwa na wanamgambo wa zamani waliojiorodhesha kupatiwa msamaha uliotolewa mwaka 2009 kwa waasi wa eneo lenye utajiri wa mafuta la Niger Delta kusini mwa nchi hiyo.
Serikali ya Abuja ilitoa ahadi hiyo jana baada ya wanamgambo hao kutishia kuanzisha tena mashambulio dhidi ya vinu na mabomba ya mafuta endapo hawatolipwa fedha walizoahidiwa.
"Tunawanasihi wote kuwa watulivu kwa kuwa malipo yote yaliyocheleweshwa na mengineyo yaliyo chini ya mpango huo yatalipwa hivi karibuni", imeeleza taarifa iliyotolewa na ofisi ya serikali inayohusika na msamaha.
Serikali ya Nigeria imekuwa ikifanya mazungumzo na wanamgambo ili wakomeshe mashambulio dhidi ya mabomba ya mafuta ghafi ambayo yalisababisha kushuka uzalishaji wa mafuta ya nchi hiyo kwa kiwango cha mapipa laki saba kwa siku kwa muda wa miezi kadhaa katika mwaka uliopita.
Chini ya mpango huo wa msamaha, kila mwanamgambo mmoja wa zamani inapasa apatiwe naira za Nigeria 65,000, sawa na karibu dola 214 za kimarekani kwa mwezi pamoja na mafunzo ya kazi.
Mwezi Novemba mwaka jana Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alikutana na viongozi wa eneo la Niger Delta pamoja na wawakilishi wa wanamgambo ili kujadili matakwa yao, lakini tangu wakati huo mafanikio madogo yamepatikana kutokana na mazungumzo hayo.
Wanamgambo na wakaazi wa eneo la Niger Delta wanataka fungu kubwa zaidi la pato linalotokana na utajiri wa mafuta ya Nigeria litengwe kwa ajili ya eneo hilo masikini.
Uuzaji mafuta ghafi unadhamini karibu asilimia 70 ya mapato ya serikali ya nchi hiyo…/