Kupinga Libya suala la kupatiwa makazi wahajiri katika ardhi ya nchi hiyo
Katika hali ambayo, Libya ingali inakabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa na kiuchumi, suala la wahajiri wanaoelekea Ulaya kupitia nchi hiyo nalo limegeuka na kuwa tatizo jingine kubwa kwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Kuhusiana na suala hilo, Fayez Mustafa al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amesisitiza juu ya upinzani wa nchi yake kwa suala la kupatiwa makazi wahajiri katika ardhi ya nchi hiyo.
Fayez al-Sarraj amesema hayo mjini Brussels katika mazungumzo yake na Didier Reynders, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ubelgiji na kueleza kuwa, Libya ni kama kivuko tu kwa wahajiri na sio chimbuko na kituo cha kuzalisha wahajiri na kuwapeleka Ulaya.
Kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini Libya na kukosekana amani na uthabiti katika nchi hiyo, kumewafanya akthari ya wahajiri na wahamiaji wa nchi mbalimbali za Kiafrika kuichagua nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kuifanya kuwa kivuko chao kwa ajili ya kuelekea Ulaya. Hii ni katika hali ambayo, Libya inakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi na ukosefu wa amani na usalama.
Ni kwa miaka sasa ambapo kutokana na kuongezeka idadi ya watu katika nchi za Kiafrika kwa upande mmoja na mazingira mabaya ya kiuchumi, ukosefu wa ajira na umasikini na vile vile vita vya ndani na harakati za makundi ya kigaidi katika akthari ya nchi za eneo kwa upande wa pili, watu wengi hususan vijana wanafanya jitihada za kuelekea barani Ulaya kwa ajili ya kutafuta maisha mazuri.
Wahajiri hao wameichagua Libya kama kivuko chepesi cha kuelekea barani Ulaya hususan Italia. Hii ni katika hali ambayo, kupita katika njia ya Bahari ya Mediterranean kuna hatari nyingi ambapo hadi sasa maelfu ya wahajiri wamepoteza maisha majini huku wengine wengi wakitumbukia mikononi mwa magenge ya biashara ya magendo ya binadamu.
Katika upande mwingine kuingia wahajiri barani Ulaya nalo limekuwa tatizo kubwa kwa nchi hizo. Kuanzia mwaka jana nchi za Ulaya zimeyafanya mazingira ya kuingia wahajiri hao katika nchi hizo kuwa magumu na zimekuwa zikiwazuia kuingia barani humo.
Kuwapatia makazi wahajiri katika mipaka ya Ulaya ni sera nyingine ambazo zinatekelezwa na viongozi wa bara hilo. Katika uwanja huo, hatua ya awali ilikuwa ni kutiwa saini makubaliano na Uturuki Machi mwaka jana. Nchi hizo za Ulaya zina mpango wa kutekeleza siasa hizo kwa nchi nyingine ulimwenguni zikiwemo akthari ya nchi za Kiafrika hususan zile zenye migogoro ya ndani. Libya kwa kuzingatia kwamba, inakabiliwa na mgogoro wa ndani, hivi sasa imegeuka na kuwa sehemu ya kukusanyika maelfu ya wahajiri wenye nia ya kuelekea barani Ulaya. Kuweko wahajiri hususan wahamiaji haramu katika vituo vya makazi na vituo vya kuwashikilia watu nchini Libya, hadi sasa kumeigharimu nchi hiyo takribani dola milioni 13 na laki tano.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linakadiria kwamba, kuna wahajiri 77 elfu nchini Libya ambapo elfu saba kati yao wanashikiliwa katika vituo vya wahajiri haramu. Hivi sasa nchi za Ulaya zipo mbioni kufikia makubaliano na Libya kwa ajili ya kuwapatia makazi wahajiri katika nchi hiyo ya Kiafrika. Kuwasimamisha na kuwazuia wahajiri katika ardhi ya Libya kunaweza kuzipunguzia kwa kiwango kikubwa nchi za Ulaya mzigo wa wahajiri wa nchi za Kiafrika wanaoelekea barani humo.
Hii ni katika hali ambayo, Serikali ya Umoja wa Kiataifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sirraj licha ya kuwa inatambuliwa kimataifa kuwa serikali halali, lakini ndani ya Libya haina uhalali na inakabiliwa na upinzani hususan wa bunge la nchi hiyo. Kwa msingi huo basi kipindi cha kutiwa saini kati ya Ulaya na Libya kinapaswa kuwa baada ya mgogoro wa ndani wa nchi hiyo kufikia tamati.
Nchi za Ulaya kama kawaida yao, zinataka kuyapatia ufumbuzi matatizo yake kupitia nchi nyingine bila kuzingatia maslahi ya nchi hizo. Hii ni katika hali ambayo, jambo ambalo ni la lazima kwanza kufanywa na nchi hizo ni kuhitimisha siasa zao za kupenda vita ambazo ndizo chanzo cha wimbi la wakimbizi na wahajiri na hivyo kulipatia ufumbuzi chimbuko kuu la matatizo hayo.