Umoja wa Mataifa: Watetezi wa haki za binadamu wanakandamizwa nchini Burundi
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusiana na vitendo vya ukandamizaji dhidi ya watetezi wa haki za binadamu huko nchini Burundi.
Michel Forst ripota wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, hali ya haki za binadamu nchini Burundi inatia wasiwasi hasa kutokana na azma ya serikali ya nchi hiyo ya kukandamiza maoni ya wapinzani. Afisa huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo zikiwa zimebakia wiki kadhaa tu kabla ya kufanyika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa Machi huko Geneva Uswisi.
Michel Forst ameeleza kuwa, taasisi kadhaa zisizo za kiserikali zimezuiwa kuendesha shughuli zao nchini Burundi na hatua hizo zimekuwa zikioshadidi kila siku.
Inaelezwa kuwa, baadhi ya maafisa wa taasisi za kiraia wamelazimika kuikimbia Burundi wakikweka
hujuma dhidi yao. Ikumbwe kuwa, Oktoba mwaka jana serikali ya Burundi ilizipiga marufuku taasisi tano za kiraia hatua ambayo imelalamikiwa vikali na Umoja wa Mataifa.
Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza, kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita, machafuko ambayo yalishika kasi zaidi mjini Bujumbura.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, zaidi ya raia 400 wameuawa nchini Burundi tangu nchi hiyo ilipotumbukia katika machafuklo huku Umoja wa Mataifa ukisema kuwa, raia laki tatu na 20 elfu wameikimbia Burundi tangu wakati huo na kuomba hifadhi katika nchi jirani.