UN na AU zamuunga mkono rais mpya wa Somalia
Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zimetangaza uungaji mkono wao kwa rais mpya wa Somalia.
Francisco Caetano, mjumbe maalumu wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Afrika na Michael Keating, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, wametangaza kwa nyakati tofauti uungaji mkono wao kwa Mohamed Abdullahi Farmajo, rais mpya wa Somalia. Kadhalika maafisa hao wa AU na UN wamemuahidi Farmajo kushirikiana naye katika kukabiliana na matatizo yanayoikabili serikali ya nchi hiyo.
Kwa upande wake Caetano, amesema kuwa, ana matumaini kwamba rais huyo mpya atashirikiana na viongozi wengine wa serikali ya Mogadishu katika njia ya umoja na amani wa Somalia ili kuweza kuyashinda matatizo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiusalama. Kadhalika mjumbe huyo wa Umoja wa Afrika nchini Somalia amewashukuru wananchi na askari wa usalama wa nchi hiyo kwa kusimamia amani katika zoezi zima la uchaguzi na kwamba ni jukumu la serikali mpya kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kudhamini usalama wa taifa hilo la pembe ya Afrika.
Farmaajo aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Somalia, alitangazwa mshindi baada ya Hassan Sheikh Mohamud aliyekuwa akitetea kiti hicho kukubali kushindwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Somalia uliowashirikisha wabunge pekee.