Wanigeria waandamana dhidi ya serikali kulalamikia hali mbaya ya uchumi nchini
Maelfu ya wananchi nchini Nigeria wamefanya maandamano katika kulalamikia siasa mbovu za kiuchumi zinazotekelezwa na serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo.
Maandamano hayo yamefanyika katika miji ya Abuja, mji mkuu wa Nigeria na Lagos, ambapo wananchi wamelalamikia uongozi mbovu wa serikali ambao umeitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Maandamano hayo yanajiri katika hali ambayo katika kampeni za uchaguzi uliomuingiza madarakani, Rais Buhari aliahidi kuboresha uchumi wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika. Buhari alitoa ahadi hizo kwa kutegemea pato la mafuta, kama ambavyo aliahidi pia kupambana na ufisadi nchini humo.
Hata hivyo baada ya kuingia madarakani bei ya mafuta katika soko la dunia iliporomoka na hivyo kuufanya uchumi wa nchi hiyo kudorora. Aidha mashambulizi ya waasi wa eneo la Niger Delta dhidi ya mashirika ya mafuta ya serikali na ya kigeni, yalipigilia msumari wa matatizo ya kiuchumi nchini humo. Katika sehemu nyingine wananchi wa Nigeria wanamtuhumu rais huyo kwa kushindwa kukabiliana na ufisadi kama alivyoahidi katika kampeni za uchaguzi.