Hatua za awali za utekelezaji wa makubaliano ya amani huko Mali
Duru mpya ya kikao cha wawakilishi wa serikali ya Mali na wapinzani kwa minajili ya kutekeleza makubaliano ya amani imefanyika kufuatia kuongezeka machafuko na vitisho vya kiusalama nchini humo.
Katika kikao hicho kati ya wawakilishi wa serikali na makundi ya wapinzani yanayobeba silaha zimepatikana njia za kufanikisha utekelezaji wa makubaliano hayo; ambapo miongoni mwake tunaweza kuashiria kutumwa vikosi vya pamoja vya kijeshi na kurejesha mfumo wa muda wa uendeshaji katika maeneo ya kaskazini mwa Mali. Vile vile kuainishwa namna miji kadhaa ya kaskazini mwa Mali itakavyosimamiwa kiuongozi ni miongoni mwa maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao hicho. Kwa mujibu wa uamuzi huo, kundi la wanamgambo wenye silaha kwa jina la CMA limepewa jukumu la kusimamia mji wa Timbuktu huku makundi yenye silaha yanayoiunga mkono serikali ya Bamako yakipewa mamlaka ya kusimamia masuala ya mji wa Gao. Wakati huo huo suala la kuwaainisha shakhsiya watakaosimamia maeneo makubwa matatu ambayo ni mji wa Kidal, Taoudenie na Menaka limeachiwa serikali ya Mali. Mali ilitumbukia kwenye mgogoro mwaka 2012 baada ya kujiri mapinduzi nchini humo.
Kujiri mapigano na kuwepo hatari inayoweza kusababishwa na mapigano hayo, yote hayo yalitoa msukumo tangu awali kwa viongozi wa serikali na wawakilishji wa makundi ya upinzani na wanamgambo wa nchi hiyo kufanya mashauriano ya kulipatia ufumbuzi suala hilo. Mashauriano hayo yalipelekea kutiwa saini makubaliano ya amani mwaka 2015 kati ya serikali ya Mali na makundi ya wapinzani.
Baada ya kusainiwa mapatano hayo, ilitazamiwa kwamba makundi ya upinzani ya wanamgambo huko Mali yangesitisha mashambulizi yake na pande mbili kujielekeza katika kurejesha amani, hata hivyo si viongozi wa serikali ya Mali wala wanamgambo hao ambao hadi sasa wameonyesha kufungamana na kuheshimu makubaliano hayo ya amani. Kinachoshuhudiwa hivi sasa huko Mali ni kushtadi mashambulizi katika maeneo ya kaskazini kuelekea katikati mwa nchi na katika maeneo mengine ya nchi hiyo. Wakati huo huo kupanuka harakati za makundi ya kigaidi katika eneo khususan kwenye mipaka ya nchi hiyo, kumebadilisha harakati za kigaidi kuwa tishio kuu kwa nchi ya Mali. Watu zaidi ya 120 waliuawa na kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa siku kadhaa zilizopita na mtu asiyefahamika aliyejilipua katika kambi ya waasi wa zamani huko Gao ambayo wanachama wake wengi ni wa kabila la Tuareg na makundi ya wanamgambo yaliyo karibu na serikali. Wapiganaji wa Kituareg zaidi ya 40 ambao ni miongoni mwa wanamgambo waliosaini makubaliano ya kusaka amani ya Mali, waliuawa katika shambulio hilo la kigaidi. Shambulio hilo kwa mara nyingine tena limeashiria kengele ya hatari kwa pande zinazozozana na kutoa msukumo mpya kwa ajili ya kuanza tena mazungumzo ya mapatano ya kitaifa.
Hadi sasa tayari zimefanyika duru kadhaa za mazungumzo kwa ajili ya kutekeleza makubaliano ya amani ya Mali kati ya wawakilishi wa serikali na wanamgambo wa nchi hiyo, hata hivyo suala la kutekeleza na kupata njia za kivitendo za kufanikisha utekelezaji wa makubaliano hayo limezingatiwa zaidi hivi sasa kufuatia kuongezeka hatari ya magaidi. Ni kwa msingi huo ndio maana kikao hicho kikapewa jina la kikao cha kuyanusuru makubaliano ya amani ya Mali. Kuhusiana na suala hilo inaonekana kuwa iwapo pande husika zitaheshimu na kutekeleza makubaliano mapya yaliyofikiwa, tunaweza kuwa na matumaini ya kurejeshwa amani huko Mali; japokuwa harakati za kigaidi na kujipenyeza baadhi ya nchi za Magharibi na hasa Ufaransa nchini humo kunafanya lengo hilo kuwa gumu.