UN yaeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya Sudan Kusini
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu machafuko na mapigano yanayoshadidi zaidi nchini Sudan Kusini.
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kimesema katika ujumbe wa siri uliotumwa kwa Baraza la Usalama la umoja huo kwamba, kushadidi mapigano katika maeneo mawili ya Wau Shilluk kwenye mkoa wa Upper Nile na Kajo Keji katika eneo la Equatoria ya Kati kutakuwa na maafa makubwa kwa raia wa maeneo hayo.
Ujumbe huo umesema kuwa, jumuiya za kutoa misaada ya kibinadamu zimesimamisha operesheni za kutoa misaada katika maeneo hayo na kwamba raia zaidi ya elfu hamisini wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo.
Baada ya Sudan Kusini kujitenga na Sudan na kuanza kujitawala mwaka 2011, kulikuwapo matumaini kwamba nchi hiyo changa ingekuwa na amani na utilivu. Hata hivyo nchi hiyo ilitumbukia katika vita ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe hapo mwaka 2013 baina ya jeshi linalomuunga mkono Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka na waasi wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kutoka kabila na Nuer .