Serikali ya Burundi kutoshiriki mazungumzo ya amani, Tanzania
(last modified Thu, 16 Feb 2017 08:00:36 GMT )
Feb 16, 2017 08:00 UTC
  • Serikali ya Burundi kutoshiriki mazungumzo ya amani, Tanzania

Serikali ya Burundi imesema haitoshiriki katika mazungumzo ya kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo yanayotazamiwa kuanza hii leo nchini Tanzania.

Phillipe Nzobonariba, Msemaji wa Serikali ya Burundi amesema kuwa, pamoja na masuala mengine, upande wa serikali umemua kutoshiriki mazungumzo hayo kulalamikia uwepo wa mshauri wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, Benomar Jamal, katika mazungumzo hayo.

Hata hivyo hajafafanua sababu za kupinga afisa huyo wa UN kushiriki mazungumzo hayo, ambayo muungano mkuu wa upinzani wa CNARED umesema kuwa utashiriki, licha ya hapo awali kususia ukimtuhumu mpatanishi mkuu, Benjamin Mkapa, Rais wa zamani wa Tanzania, kuwa anaegemea upande mmoja.

Benjami Mkapa alipokuatana na Rais Nkurunziza mwaka jana, Bujumbura

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hata kabla ya kuchukua rasmi hatamu za uongozi, alimtumia ujumbe wa maandishi Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi na kubainisha kuwa UN iko tayari kushiriki kwa dhati katika juhudi za kuupatia suluhisho mgogoro wa ndani wa Burundi. 

Wiki iliyopita, Michel Forst ripota wa Umoja wa Mataifa  alitangaza kuwa, hali ya haki za binadamu nchini Burundi inatia wasiwasi hasa kutokana na azma ya serikali ya nchi hiyo kukandamiza maoni ya wapinzani na watetezi wa haki za binadamu.

Machafuko na umwagaji damu ulianza kushuhudiwa nchini Burundi mwezi Aprili mwaka 2015 na kushtadi baada ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuamua kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo, hatua ambayo wapinzani wanasema ni kinyume na katiba na makubaliano ya amani yaliyofikiwa mjini Arusha, Tanzania.