Vikao vya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya na changamoto zilizopo
Juhudi za kieneo na kimataifa za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya zingali zinaendelea huku kukiwa hakuna kikao chochote kati ya vilivyofanyika ambacho hadi sasa kimeweza kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo. Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, Algeria na Misri kwa mara nyingine tena wanatazamiwa kukutana huko Tunisia kujadili njia za kukomesha mgogoro wa miaka sita wa Libya.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imetangaza kuwa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo tatu watafanya mazungumzo hayo ili kujadili njia kuu za kisiasa za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya. Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imesema, kikao hicho kinafanyika ikiwa ni katika juhudi za kuyakutanisha pamoja makundi hasimu ya Libya kwenye meza ya mazungumzo.
Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na Jenerali Khalifa Haftar, Kamanda wa vikosi vya Libya mashariki mwa nchi hiyo wiki iliyopita walitarajiwa kufanya mazungumzo katika kikao kilichoitishwa na Misri huko Cairo kujadili vipengee vya makubaliano yaliyosainiwa nchini Morocco mwezi Disemba mwaka 2015. Makubaliano hayo yalisainiwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa; na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imeundwa kwa kutegemea vipengee hivyo. Libya iligawanyika katika maeneo mawili ya mashariki na magharibi kufuatia uingiliaji wa kisiasa na kijeshi wa baadhi ya nchi za Kiarabu na za Magharibi hasa baada ya kupinduliwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011. Hii ni katika hali ambayo vita vya kuwania madaraka kati ya makundi ya kisiasa nchini humo vingali vinaendelea hadi leo hii. Vita hivyo vimeongeza hatari ya kugawanyika zaidi Libya, hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo hivi sasa imegeuzwa kuwa njia ya kupitishia makundi ya kitakfiri, kuvushia silaha na wahajiri wanaoelekea barani Ulaya.
Vikao mbalimbali katika ngazi ya kieneo na kimataifa vya kutatua mgogoro wa Libya vimekwishafanyika tangu kuanza mgogoro wa kisiasa nchini humo. Hata hivyo hadi kufikia sasa hakujapatikana njia ya kivitendo ya kuhitimisha mapigano na kurejesha amani huko Libya isipokuwa kufikiwa maamuzi kadhaa tu ikiwemo suala la uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo. Wakati huo huo sababu mbalimbali zimejumuishwa katika kuendelea hali ya mgogoro huko Libya na kufeli vikao mbalimbali vya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo. Sababu hizo zinaweza kugawanywa katika makundi mawili. Kuweko makundi mengi ya kisiasa, kuweko makabila na kaumu tofauti na mashinikizo ya makabila hayo ya kutaka kushirikishwa katika hatamu za uongozi, kuwa na udhibiti, na pia kuwepo mitazamo ya kisiasa inayokinzana, yote hayo yamesababisha kushindwa na kukosekana utaalamu wa kutosha wa kuendesha nchi; kiasi kwamba wanamgambo sasa ndio wanaodhibiti na kuwa na mamlaka ya uendeshaji katika maeneo mengi ya Libya. Aghlabu ya wanamgambo hao wanaungwa mkono na nchi za eneo hilo. Vita hivyo vya kuwania madaraka vimepelekea kushindwa kushiriki katika mazungumzo nje ya nchi baadhi ya makundi yenye taathira na hivyo kukwamisha juhudi za kuchukua uamuzi wa pamoja wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo. Katika upande mwingine, vita vya kuwania madaraka na kutaka kushirikikwa serikalini makundi hayo vingali vinaendelea nje ya nchi hiyo. Hata kama washiriki wa vikao mbalimbali vya kutatua mgogoro wa Libya kidhahiri wanaonekana wanatafuta njia za kumaliza mgogoro wa nchi hiyo, lakini ukweli ni kuwa matarajio yaliyopo na mashinikizo ya makundi ya wanamgambo ya kutaka kupewa madaraka serikalini, na vile vile kuwepo mchuano juu ya namna ya kufaidika na maliasili za Libya, ni mambo ambayo yameyafanya mazungumzo ya Libya kuwa magumu.