Amnesty yaikosoa serikaliya Nigeria kwa kutozingatia sheria
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeikosoa vikali serikali ya Nigeria kwa kutoheshimu sheria.
Isa Sanusi Mkurugenzi wa Habari wa Amnesty International kitengo cha Nigeria amesema, hatua ya serikali ya rais Mohammadu Buhari wa Nigeria ya kukataa kuheshimu amri ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo iliyotaka aachiliwe huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky ni ishara ya wazi kuwa serikali ya nchi hiyo inapuuza sheria.
Kuhusu hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky, Sanusi amesema yamkini mwanazuoni huyo wa Kiislamu amepoteza uwezo wa kuona na sasa ni kipofu.
Hivi karibuni pia, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeitahadharisha serikali ya Rais Muhammad Buhari wa nchi hiyo kutokana na ukwamishaji inaofanya kuhusiana na suala la kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Itakumbukwa kuwa Sheikh Zakzaky akiwa na mke wake alitiwa mbaroni na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 katika kituo cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.
Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ya kiafya si nzuri, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.