Machafuko yachachamaa Nigeria, serikali yapiga marufuku watu kutoka nje
-
Samuel Aruwan, msemaji wa mkuu wa jimbo la Kaduna la kaskazini mashariki mwa Nigeria
Machafuko ya kikabila yamepamba moto kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuilazimisha serikali ya nchi hiyo kutoa amri ya kutotoka nje kwa masaa 24 katika maeneo yenye machafuko.
Televisheni ya Sky News imemnukuu Samuel Aruwan, msemaji wa mkuu wa jimbo la Kaduna la kaskazini mashariki mwa Nigeria akisema jana usiku kuwa, watu 14 wameshauawa kutokana na machafuko ya kikabila kwenye baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, hivyo serikali imelazimika kupiga marufuku watu kutoka nje kwa masaa 24.
Taarifa zinasema kuwa, wafugaji na wakulima Waislamu na Wakristo wanapigana kugombania maeneo ya malisho na vyanzo vya maji na hivyo kuiweka kwenye wakati mgumu serikali ya Nigeria.
Wakati huo huo Aghole Abeh, mkuu wa jeshi la polisi la jimbo la Kaduna, kaskazini mashariki mwa Nigeria amesema, jeshi hilo limetuma askari wake maalumu wa kupambana na ghasia kwenye maeneo ya machafuko.
Kwa mujibu wa takwimu za asasi ya kitaifa ya kukabiliana na migogo nchini Nigeria, zaidi ya watu 200 wameshauawa katika machafuko ya kusini mwa jimbo la Kaduna tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017. Habari hizo zimeongeza kuwa, watu 800 wamepoteza maisha yao katika machafuko ya jimbo la Kaduna tangu mwaka 2011.