Kivuko cha mpaka wa Cameroon na Nigeria chafungwa; wasiwasi watanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25580-kivuko_cha_mpaka_wa_cameroon_na_nigeria_chafungwa_wasiwasi_watanda
Kivuko cha mpaka baina ya nchi mbili jirani za Cameroon na Nigeria kimefungwa kutokana na sababu za kiusalama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 24, 2017 10:40 UTC
  • Kivuko cha mpaka wa Cameroon na Nigeria chafungwa; wasiwasi watanda

Kivuko cha mpaka baina ya nchi mbili jirani za Cameroon na Nigeria kimefungwa kutokana na sababu za kiusalama.

Vyombo vya usalama vya Cameroon vimesisitiza kuwa, serikali ya nchi hiyo imechukua uamuzi wa kukifunga kivuko cha mpaka baina yake na Nigeria cha mji wa Fotokol kufuatia shambulio la jana la wanamgambo wa Boko Haram katika kituo cha upekuzi cha mji wa Gambaru.

Duru za usalama za cameroon zimetangaza kuwa, wanajeshi wengi wametumwa katika mji wa Fotokol kwa ajili ya kusimamia usalama kutokana na kushuhudiwa mashambulio ya mara kwa mara ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Kivuko cha mpakani cha Fotokol ambacho kinahesabiwa kuwa sehemu ya kupitishia bidhaa za biashara baina ya Cameroon, Chad na Nigeria mwaka 2015 kilifungwa pia, na Oktoba mwaka jana kilifunguliwa na kuanza shughuli zake kama kawaida. 

Kufungwa kwa kivuko hicho kumekuwa kukikwamisha pakubwa biashara kati ya nchi tatu za Nigeria, Chad na Cameroon.

Kundi la Boko Haram lingali linaendeleza mashambulizi na milipuko ya mabomu katika maeneo mbalimbali  huko Cameroon, khususan katika mkoa wa kaskazini mwa nchi hiyo. Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa Cameroon ni nchi ya pili baada ya Nigeria iliyoathiriwa na mgogoro wa Ziwa Chad uliosababishwa na magaidi wa kitakfiri wa Boko Haram.