UN yatoa indhari: Hali ya kibinadamu Sudan Kusini inazidi kuwa mbaya
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini inazidi kuwa mbaya na kutoa wito wa kurahisisha ufikishaji misaada katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko na ya watu wenye ukata wa maisha.
Eugene Owusu, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ametoa taarifa akizitaka pande zote husika katika mgogoro wa nchi hiyo kutoa fursa ya kuwezesha kufikishwa kwa haraka na kusambazwa kwa urahisi misaada ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Taarifa ya mratibu wa misaada ya kibinadamu wa UN nchini Sudan Kusini imebainisha kuwa wakaazi wa maeneo mengi ya nchi hiyo wanaishi katika hali na mazingira magumu kimaisha.

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zinazopigana nchini Sudan Kusini kuzingatia hali za wafanyakazi wa kimataifa wa ufikishaji misaada ya kibinadamu katika hali ambayo, mnamo wiki za karibuni baadhi ya matukio ya kiusalama yametatiza na hata kukwamisha operesheni za ufikishaji misaada ya kibinadamu nchini humo.
Machafuko na kushindwa mashirika ya misaada ya kibinadamu kuyafikia maeneo yaliyoathiriwa na machafuko na yenye ukata nchini Sudan Kusini kumehatarisha maisha ya karibu watu laki moja wa baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na ukame na njaa nchini humo.

Sudan Kusini, ambayo ilijitangaza kuwa taifa huru mwaka 2011, tangu mwezi Desemba 2013 imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Licha ya kutumwa walinda amani 12,000 wa kimataifa nchini humo makumi ya maelfu ya watu wameshauawa hadi sasa na zaidi ya wengine milioni tatu wamelazimika kuyahama makaazi yao na kuwa wakimbizi.
Vita hivyo vya ndani vinahusisha jeshi tiifu kwa Rais Salva Kiir na wapiganaji watiifu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais Riek Machar.../