Safari ya ujumbe wa Baraza la Usalama Barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26020-safari_ya_ujumbe_wa_baraza_la_usalama_barani_afrika
Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameanza safari ya kuzitembelea nchi nne za eneo la Ziwa Chad. Safari hiyo inafanyika huku eneo hilo likisumbuliwa na changamoto kubwa ya ugaidi na tatizo la wimbi kubwa la wakimbizi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Mar 06, 2017 10:27 UTC
  • Safari ya ujumbe wa Baraza la Usalama Barani Afrika

Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameanza safari ya kuzitembelea nchi nne za eneo la Ziwa Chad. Safari hiyo inafanyika huku eneo hilo likisumbuliwa na changamoto kubwa ya ugaidi na tatizo la wimbi kubwa la wakimbizi.

Lengo la safari hiyo limetajwa kuwa ni kuchunguza mgogoro wa eneo la Ziwa Chad na kuelekeza macho ya walimwengu katika matatizo ya eneo hilo. 

Mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram yamevuruga maisha ya raia katika nchi za eneo la Ziwa Chad. Katika kipindi cha miaka saba iliyopita mashambulizi ya kundi hilo yameua maelfu ya watu wasio na hatia na kulazimisha wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi.

Wakimbizi eneo la Ziwa Chad

Nigeria ndiyo iliyoathiriwa zaidi na mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi. Raia wengi wa nchi hiyo hususan katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki wamekimbia makazi na nyumba zao na kuishi katika hali ngumu. Mashambulizi hayo pia yamewalazimisha maelfu ya raia kukimbilia katika nchi jirani au maeneo mengine yenye usalama na amani. Idadi kubwa ya raia hao sasa wanaishi katika kambi za wakimbizi wakisumbuliwa na uhaba wa chakula na huduma za afya. Mbaya zaidi ni kuwa makundi ya kutoa misaada ya kibinadamu hayawezi kufika katika maeneo yaliyoathiriwa na mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi kutokana na hali mbaya ya usalama. Kwa sababu hiyo kuna wasiwasi kwamba baadhi ya wakimbizi hao wanakabiliwa na hatari ya kifo. Hali hiyo mbaya ya wakimbizi inashuhudiwa pia katika nchi za Niger, Cameroon na Chad. 

Wakimbizi waliofurushwa makwao na kundi la Boko Haram

Sambamba na safari ya ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika nchi za eneo la Ziwa Chad, jumuiya na mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yametahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea maafa makubwa katika eneo hilo. Wakati huo huo ripoti zinasema kuwa hadi sasa hakujatolewa misaada ya aina yoyote ya kimataifa kwa ajili ya mgogoro wa eneo hilo. Baadhi ya nchi kubwa za Magharibi hususan Marekani zinazojigamba kutetea haki za binadamu hazikutenga bajeti katika mkutano wa kimataifa wa Oslo kwa ajili ya kuwasaidia wanadamu wanaoteseka kaskazini mwa Nigeria. Katika mkutano huo wa kimataifa nchi 14 ziliahidi kutoa msaada wa dola milioni 672 katika kipindi cha miaka 3 ijayo kwa ajili ya kuzisaidia nchi za eneo la Ziwa Chad. Hata hivyo ahadi hiyo bado haijatekelezwa kivitendo.

Raia wa kawaida ndio wanaoathiriwa na mashambulizi ya Boko Haram

Alaa kulli hal, wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, mgogoro wa sasa katika eneo la Ziwa Chad ni matokeo ya siasa za kindumakuwili za nchi za Magharibi hususan Marekani. Wachambuzi hao wanasema nchi hizo zimekuwa zikiyasaidia makundi ya kigaidi kama Boko Haram kwa siri kwa shabaha ya kudumisha machafuko na kutumia hali hiyo kama kisingizio cha kuingilia mambo ya ndani ya nchi za eneo hilo. Kwa sababu hiyo mapambano dhidi ya kundi hilo la kigaidi yamekuwa magumu na kuchukua muda mrefu na raia wa kawaida ndio wanaoendelea kuteseka kutokana na siasa hizo chafu za madola ya Kimagharibi.