Watu 36 wauawa na kujeruhiwa waking'ang'ania chakula Zambia
(last modified Tue, 07 Mar 2017 07:10:11 GMT )
Mar 07, 2017 07:10 UTC
  • Watu 36 wauawa na kujeruhiwa waking'ang'ania chakula Zambia

Kwa akali watu wanane wamepoteza maisha huku wengine 28 wakijeruhiwa katika mkanyagano na msongamano waking'ang'ania chakula cha msaada nchini Zambia.

Taarifa ya polisi ya Zambia imesema kuwa, mkasa huo ulitokea jana Jumatatu katika uwanja wa michezo wa Olympic Youth Development Centre katika mji mkuu Lusaka, ambapo watu zaidi ya 35,000 walikuwa wamekusanyika kupokea chakula cha msaada. 

Memory Chisanga, mwanamke mwenye umri wa miaka 64 ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, hali ngumu ya maisha ndiyo iliyomsukuma kwenda katika uwanja huo kupokea chakula cha msaada bila kujali umri wala jinsia yake.

Wazambia wakisubiri chakula cha msaada mwaka jana 2016

Zambia ambayo ina takriban watu milioni 14.5, ni moja ya nchi za Kiafrika ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimekumbwa na changamoto mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Takwimu na ripoti za mashirika ya kimataifa zinaonesha kuwa, zaidi ya watu milioni 40 katika nchi nyingi za Afrika wameathiriwa na njaa na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama El Nino.

Hapo jana Waziri Mkuu wa Somalia, Ali Khaire alitangaza kuwa, njaa iliyolikumba eneo la Bay huko kusini magharibi nwa nchi imeua watu wasiopungua 110 katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita. 

Tags