Magaidi wawili wanawake wauawa kaskazini mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26302-magaidi_wawili_wanawake_wauawa_kaskazini_mwa_nigeria
Magaidi wawili wanawake wanaoaminika ni wanachama wa kundi la wakufurishaji la Boko Haram wameuawa katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2017 14:57 UTC
  • Magaidi wawili wanawake wauawa kaskazini mwa Nigeria

Magaidi wawili wanawake wanaoaminika ni wanachama wa kundi la wakufurishaji la Boko Haram wameuawa katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Televisheni ya Press TV imemnukuu msemaji wa jeshi la Polisi la Nigeria, Victor Isuku akitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, magaidi hao wana umri wa takriban miaka 18 na walikusudia kushambulia wanajeshi wa Nigeria. 

Duru za Shirika la Taifa la Kusimamia Hali ya Dharura nchini Nigeria (NEMA) zimesema kuwa, mmoja wa wanawake hao wawili waliouawa, alikuwa mja mzito. Maafisa wengine wa mashirika ya uokoaji wamesema kuwa, mshambuliaji mmoja amejeruhiwa katika tukio hilo, hata hivyo hawakusema iwapo washambuliaji hao wamefanikiwa kuripua au la.

 

Taarifa zinasema kuwa washambuliaji hao walijaribu kujipenyeza mjini Maiduguri ambao ni makao makuu ya jimbo la Borno. Jimbo hilo wakati fulani lilikuwa ngome ya kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo linatuhumiwa kutoa mafunzo kwa watoto wadogo, wasichana na vijana ili wafanye mashambulizi ya kigaidi. Watu kadhaa waliuawa mwezi Januari mwaka huu baada ya mwanamke mmoja aliyekuwa amebeba mtoto kujiripua katikati ya kundi la watu huko Borno.

Kundi la Boko Haram liliua raia wasiopungua 117 katika kipindi cha mwezi Februari 2015 hadi Septemba 2016 na kuwalazimisha raia karibu laki tatu kuyakimbia makazi yao.

Watu wasiopungua 20 elfu wameshauawa katika kipindi cha zaidi ya miaka saba ya mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram huko Nigeria na katika nchi jirani kama vile Chad, Cameroon na Niger.