Safari ya Waziri Mkuu wa Libya nchini Sudan yaakhirishwa
-
Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.
Ziara ya Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya nchini Sudan imeakhirishwa kutokana na matukio ya kiusalama nchini humo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeripoti kuwa Mohammed al Taher Siyala, Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya amezungumza kwa njia ya simu na Ibrahim Ghandour waziri mwenzake wa Sudan na pande mbili hizo zimejadiliana matukio ya kiusalama yanayojiri huko Libya hususan katika mji mkuu Tripoli na kueleza kuwa, matukio hayo yamepelekea kuakhirishwa ziara ya Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya mjini Khartoum.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Mohammed al Taher amesisitiza pia kuwa, serikali ya Libya inapendelea kuona Waziri Mkuu wa nchi hiyo anafanya ziara mjini Khartoum katika siku chache zijazo.
Mapigano kati ya wanamgambo wenye mfungamano na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya na makundi yanayobeba silaha yameshika kasi tangu jana Jumanne katika maeneo mawili ya al Andalus al Kubrah na Farji; huku mapigano yakiripotiwa kuendelea pia katika eneo la Hilali ya Mafuta huko kaskazini mashariki mwa Libya.