NASA yatakiwa kutumia mfumo wa mlolongo kumteua mgombea urais Kenya
Muungano wa upinzani wa NASA nchini Kenya umetakiwa kutumia mfumo wa upigaji kura wa mlolongo kumteua mgomea kiti cha urais.
Pendekezo hilo limetolewa na Hassan Mwanyoha, mbunge wa Matuga katika Kaunti ya Kwale katika eneo la Pwani katika mahojiano maalumu na Radio Tehran pamoja na tovuti ya parstoday.com/sw.
Katika mfumo wa upigaji kura wa mlolongo, wapiga kura hupanga foleni nyuma ya picha ya mgombea wamtakaye. Wakiwa katika foleni huhesabiwa na baada ya hapo idadi ya watu waliosimama nyuma ya picha hutangazwa rasmi.
Katika mahojiano aliyofanya na Mubarak Henia akiwa safarini mjini Tehran hivi karibuni, aidha aliwataka vinara wa NASA waache tamaa na wawe tayari kujitolea ili kufanikisha malengo ya upinzani.
Muungano huo wa NASA unaendelea kukumbwa mgogoro kuhusu nani atakayepeperusha bendera ya muungano huo kukabiliana na chama tawala cha Jubilee mwezi Agosti mwaka huu.
Kukosekana muafaka miongoni mwa wagombea wanne wa muungano huo ambao ni Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa ANC, Raila Odinga wa ODM na Moses Wetangula wa Ford Kenya kumeibua hali ya taharuki miongoni mwa wafuasi wa vinara hao. Kuna wasiwasi kuwa huenda muungano huo ukasambaratika jambo ambalo limepelekea wafuasi wa NASA kuanza kutoa mapendekezo mbali mbali ili kuunusuru.